Mawakili wanne wajitokeza kumtetea Lulu



JOPO la mawakili wanne maarufu nchini akiwamo Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De Mello, wamejitokeza kumtetea msanii wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta Lulu anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa msanii maarufu Steven Kanumba.
De-Mello ambaye pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King, anaungana na wanasheria wengine ambao ni Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe katika kumtetea Lulu mwenye umri wa miaka 17.
Fungamtama ambaye ndiye kiongozi wa jopo lao anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans katika kesi dhidi ya Shirika la Umeme la Tanzania (Tanesco).
Katika kesi hiyo Dowans ilishinda na Tanesco iliamuliwa kuilipa Dowans zaidi ya Sh 94 bilioni kwa kuvunja mkataba kinyume cha sheria.


Kwa upande wake, Kibatala ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe, katika kesi ya uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wakati Massawe anatoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Mawakili hao walijitokeza  Jumatatu, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Ritha Tarimo, kwa ajili ya kumtetea Lulu anayekabiliwa na kesi ya hiyo ya mauaji. Kesi hiyo ilikuja mahakamani hapo jana kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya mawakili hao kujitambulisha kumtetea msanii huyo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine.

Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Lulu alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi kwa kutumia gari la Magereza lenye namba za usajili STK 4310 ambalo lilisindikizwa na gari mbili zenye usajili namba STK 4253 na STK 8901.

Alikuwa chini ya ulinzi mkali wa askari sita wa kike wa Jeshi la Magereza pamoja na askari mmoja wa kike wa Jeshi la Polisi.
Askari hao kwa kushirikiana na askari wa kiume wa Jeshi la Magereza zaidi ya sita walimwingiza msanii huyo mahakamani kwa ulinzi mkali kiasi kilichowafanya baadhi ya wapiga picha kushindwa kumwona.

Lulu ambaye alikuwa amevalia vazi la aina ya dira la rangi nyekundu, kutokana na kubanwa katikati ya askari hao wakati akiingizwa mahakamani, alianza kulia kitu ambacho kilimfanya Hakimu Tarimo kumpa pole na baadhi ya askari kumnyamazisha.

Kutokana na kujaa kwa watu mahakamani humo na wengine wakitaka kuzidi kuingia askari wa jeshi la Magereza walitumia nguvu kufunga mlango wa chumba cha mahakama hiyo na kuwezesha kesi hiyo kusikilizwa.

Baada ya kesi hiyo kumalizika, wakili Kaganda, aliiomba mahakama iamuru watu wote watoke nje ili mtuhumiwa aweze kupitishwa kwa sababu walikuwa wamefunga njia.

Kufuatia ombi hilo, hakimu Tarimo aliwaamuru askari kusafisha njia ili waweze kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa na anaweza kuumizwa.

"Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisisitiza Hakimu Tarimo.

Baada ya kutolewa kwa amri hiyo askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Lulu kufikishwa mahakamani hapo. Mara ya kwanza ilikuwa Aprili 10 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando.

Wakati akifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, polisi walitumia mbinu za kikachero kuwapiga chenga waandishi ambao wengi walikwenda mahakama ya Kinondoni wakidhani mtuhumiwa huyo angefikishwa hapo, lakini akapandishwa Kisutu na kusomewa mashtaka katika kipindi kisichozidi dakika kumi kisha kupelekwa rumande.

Pia tofauti na matarajio, siku hiyo polisi hawakuwa wametumia magari yenye ving'ora na ulinzi wa kutisha kama ilivyotarajiwa bali walitumia magari mawili madogo na alipofika mahakamani hapo, alisomewa shitaka hilo na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda.

Kaganda akimsomea hati ya mashtaka Lulu, alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu, maeneo ya Sinza Vatican katika wilaya ya Kinondoni, Lulu alimuua, Steven Kanumba.

Baada ya kumaliza kusoma shtaka hilo, Kaganda alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hata hivyo, Lulu hakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina uwezo wa kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu.

Hakimu Mmbando aliamuru Lulu apelekwe rumande katika Gereza la Segerea kwa sababu shtaka linalomkabili ni moja kati ya mashtaka yasiyo na dhamana.

Kanumba alifariki dunia usiku wa Aprili 7 kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake na Lulu. Alizikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.