SHIBUDA: HAKUNA URAIS BILA KUCHAGULIWA NA CCM


MBUNGE wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda ameeleza kuwa aliamua kutangaza nia ya kugombea urais Chadema kupitia vikao vya CCM kwa sababu anatambua kuwa hakuna mwanachama wa chama chake anayeweza kuwa Rais bila kuchaguliwa na chama hicho tawala.


Hata hivyo, jana Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limemshukia na kumtaka aeleze anafanya nini katika chama hicho kama anaamini kuwa hakiwezi kushika dola.

Shibuda alikaririwa na vyombo vya habari jana akieleza kuwa anataka kugombea urais kupitia Chadema na kumwomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwa meneja wake.

Jana, alipotakiwa kufafanua zaidi mantiki ya kauli yake hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha mada kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) mjini Dodoma, Shibuda alisema anataka kuwa Rais wa Watanzania wote hivyo, hata kura za CCM anazihitaji ndiyo maana akatangaza mbele ya jukwaa lao.

 

Shibuda alisema hakuna mwanachama wa Chadema anayeweza kuwa Rais wa nchi hii bila kupata kura za baadhi ya wanachama wa CCM na Watanzania wengine: “Hata katika hayo majimbo ambayo Chadema tumeshinda, hatukupigiwa kura na wanachama wa Chadema pekee, bali walikuwepo hadi wa CCM wanaopenda mageuzi.


"Mimi ni ‘field marshal’ katika siasa. Ndiyo, nimetangaza mbele ya jukwaa la CCM kwa sababu nahitaji kura zao. Nahitaji kura ya Kikwete na wana CCM wengine, mimi siyo mtu mwoga wa kutangazia vichochoroni Kariakoo," alitamba Shibuda na kuongeza:

“Mtu pekee mwenye boresho la kisiasa ni Shibuda. Mimi ndiye ninayeweza kujenga umoja na kutimiza malengo ya nchi. Ndiyo maana nilimwambia Rais Kikwete sasa ni zamu yangu na nitakangaza mbele ya jukwaa la CCM siyo kujificha vichochoroni Kariakoo.”

Shibuda akitetea msimamo wake, alisema si dhambi kwa mhadhiri wa Kiislamu kwenda kutoa mahubiri ya kutoa uchafu wa roho mbele ya jukwaa la Wakristo vivyo hivyo, kwa mhadhiri wa Kikristo kwenda kutoa mahubiri kwenye jukwaa la Waislamu na kuhoji: “Kuna uharamu gani au je, ni usaliti kwa dini yake?”

“Tuache fikra finyu. Shibuda anataka kuwa Rais wa Watanzania wote. Wanaosema kwa nini nimeongea kwenye jukwaa la CCM wana fikra finyu. Mimi nina maono mapana ya kitaifa. Kwani hata watu waliotalakiana bado wanashirikiana kwenye misiba na harusi, wanakutana na kusalimiana na hawana ugomvi wowote, hao ndiyo watu wastaarabu. Tuache kuzusha mambo kwa hisia hasi.”

“Mfumo wa vyama vingi siyo uadui. Mimi nitakuwa Rais bora mwenye maono mapana ya kitaifa. Mimi ni sawa na gogo la udi likichomwa linatoa manukato. 


Nitaendelea kutangaza msimamo wangu na kuomba kura hata nikiwa katika jukwaa la NCCR-Mageuzi, CUF na vyama vingine kwani mimi nataka kuwa Rais wa Watanzania wote siyo wa kabila fulani au watu fulani. Mimi sibagui dini, kabila wala rangi. Watu waache fikra na mawazo mgando.”

Kauli ya Bavicha
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche  imesema baraza hilo limepokea kwa mshtuko taarifa kwamba Shibuda atagombea urais na meneja wake wa kampeni atakuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na alitoa kauli hiyo kwenye kikao cha Nec ya CCM.

Pia wameshtushwa na kitendo cha Shibuda kusema kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuiongoza nchi kwa sasa na kutoa tamko hilo kwa niaba ya Taasisi inayotathmini Utawala Bora Afrika (APRM).

“Mambo hayo manne ndiyo yametushtua na kutufedhehesha sisi vijana wa Chadema na ndiyo maana, tumelazimika kutoa kauli kuhusiana na suala hili,” alisema Heche.

Heche alisema kamwe Bavicha haitaruhusu mgombea urais wa Chadema kuwa na meneja wa kampeni kutoka CCM akisema kina watu wa kutosha na wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo.

“Kamwe hatutaruhusu mgombea urais wa Chadema awe anatangaza nia kwenye vikao vya CCM, kwani hawana mamlaka ya kumteua mgombea wa Chadema na kama Shibuda alikuwa halijui hilo anapaswa kulifahamu kuanzia sasa kuwa vijana wa Chadema hatuchaguliwi mgombea na Nec ya CCM kwani Chadema kuna vikao na taratibu zetu za kuteua wagombea,” alisema Heche.

Alisema kitendo cha Shibuda kusema kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi ni kudhalilisha  vijana wa Chadema na Watanzania wote ambao leo wanakiona chama hicho kama tumaini pekee la kuwakomboa.

“Kwa kauli hii, tunaamini kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya bila kutakiwa maelezo ya kina. Tutaitisha kikao cha Baraza na tutaijadili kauli hii na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama,” alisema na kuongeza:

“Kwa nini atafute urais kwenye chama ambacho anaona hakiwezi kuongoza dola? Anawatania Watanzania? Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza dola. Kwani lengo la chama chochote kile ni kuchukua dola na si vinginevyo.”



Mwananchi