Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika mazungumzo na Askofu Mkuu Protase Rugambwa Ikulu
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipata picha ya kumbukumbu na Askofu Mkuu Protase Rugambwa
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Askofu
Mkuu Protase Rugambwa baada ya mazungumzo yao.
Askofu
wa Jimbo la Kigoma la Kanisa Katoliki, Baba Askofu Protase Rugambwa
amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete kwa sera nzuri ambazo zimeuwezesha Mkoa wa Kigoma kupata
miundombinu nyingi na muhimu katika kipindi kifupi.
Aidha,
Askofu Rugambwa amesema kuwa hana shaka kuwa kwa mipango iliyopo ya
Serikali ni dhahiri kuwa Mkoa wa Kigoma utakuwa unapaa kwa maendeleo
hasa baada ya kuanza kufanya kazi kwa eneo la uzalishaji wa kiuchumi kwa
ajili ya kuuza nje la EPZ.
Askofu
Rugambwa ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 26, 2012 wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Kikwete katika mkutano
uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
“Sina shaka kuwa kuanzishwa kwa EPZ kutabadilisha kabisa kasi ya maendeleo ya Mkoa wa kigoma na hali ya wananchi wa Mkoa huo,”
amesema Baba Askofu Rugambwa ambaye pia amemshukuru Rais Kikwete kwa
salamu zake za pongezi kufuatia uteuzi wa kushika nafasi kubwa zaidi ya
uongozi wa Kanisa Katoliki kwenye makao ya Kanisa hilo mjini Vatican.
Mwezi
uliopita, Kiongozi wa Kanisa katoliki, Baba Mtakatifu Papa Benedict wa
XV1 amemteua Askofu Rugambwa kuwa Katibu Mwambata (Adjunct) wa
Kongregasio ya Uenezaji wa Injili kwa Ajili ya Mataifa na Rais wa
Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, Roma.
Aidha,
kufuatia uteuzi huo, Papa Benedict wa XV1 amempandisha daraja Askofu
Rugambwa na kumfanya Askofu Mkuu. Baba Askofu Rugambwa anachukua nafasi
iliyoachwa wazi na Askofu Mkuu Pierqiuseppe Vacchelli ambaye Baba
Mtakatifu amekubali kujiuzulu kwake nafasi hiyo baada ya kufikisha umri
wa kustaafu.
Askofu
Rugambwa amemwambia Rais Kikwete kuwa atapanga kuondoka nchini mwezi
ujao Agosti 27 kwenda Vatican tayari kuanza kazi yake mpya.
Rais
Kikwete kwa mara nyingine amempogeza Askofu Rugambwa kwa uteuzi wake
akimwambia kuwa kitendo na uamuzi wa Baba Mtakatifu umeiongezea Tanzania
heshima. “Uteuzi huu ni heshima kwako na kwa nchi yetu.”
Rais
Kikwete amemwambia Askofu Rugambwa kuwa ni furaha kwa Tanzania kwa
kadri wananchi wake wanavyozidi kupata nafasi za utumishi wa kimataifa.
Kuhusu
mipango ya maendeleo ya Kigoma, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali
yake ingependa kuufanya mkoa huo, kama ilivyo mingine, mambo makubwa
zaidi lakini bajeti ya serikali haitoshelezi kufanya kila kitu kwa
wakati mmoja.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Julai, 2012