"SERIKALI PEKEE HAIWEZI KUKOMESHA MMOMONYOKO WA MAADILI.....MASHIRIKA HUSIKA NA VIONGOZI WA DINI WASHIRIKIANE".......WAZIRI SIMBA


WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Sophia Simba amekuja juu akisema mmomonyoko wa maadili katika jamii ndiyo unaochangia kwa sehemu wana ndoa kufumaniana kila kukicha.

Akizungumza na gazeti hili, juzikati jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Simba alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, viongozi wa dini nao wanahusika sana kwani wakiwa kwenye mimbari zao hawaneni na waumini wao kuhusu dhambi hiyo kuu ya usaliti.
 

****************
 “Kwanza vitendo vya kufumaniana vinaathiri watu kisaikolojia na kuharibu uhusiano kati ya mke na mume, hivyo kusumbua watoto endapo wana ndoa hao watakuwa wamefanikiwa kuwa nao,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Waziri Simba alisisitiza kuwa tatizo la wana ndoa kufumaniana ni kubwa na sasa linazidi kuota mizizizi kutokana na watu kutozingatia maadili ya Kitanzania na yao wenyewe.

“Katika hili, serikali haiwezi kukomesha tatizo, bali taasisi husika, mashirika mbalimbali yanayojishughulisha na masuala ya maadili wakiwemo viongozi wa dini, wote washirikiane kwa pamoja  ili kuweza kutoa elimu ya kiroho kwa wananchi na kuwaambia madhara ya dhambi hiyo,”
alisema.




Pia waziri huyo aliitetea serikali iliyopo madarakani akitaka isibebeshwe mzigo wa lawama kuhusu hilo.

“Kuna mambo ambayo serikali inaweza kufanya yenyewe na mengine lazima kushirikisha taasisi zingine kwa hiyo katika hili serikali isibebeshwe mzigo wa lawama hata kidogo.”  

Aliongeza kuwa suala la mapenzi kufanywa hovyohovyo ni hatari na ndiyo maana mtu anapofikia umri wa kuoa au kuolewa hufanya hivyo kwa lengo la kujenga familia badala ya kuzungukazunguka.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wetu umebaini kuwa wana ndoa ndiyo wanaongoza kwa kufumaniana kuliko wachumba au wapenzi japo imani hazikubaliani na makundi hayo kukutana kimwili kabla ya ndoa.

Katika Jiji la Dar es Salaam peke yake, inakadiriwa kuwa kila baada ya siku mbili kunatokea fumanizi kwenye vitongoji vyake huku wanaume wakiongoza kwa kufumaniwa wakiwa na wanawake wengine.

Utafiti zaidi umegundua kuwa, mafumanizi mengi ya miaka ya karibuni yanachangiwa na simu za mkononi, hasa watu kupanga usaliti kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu ‘SMS’.

Aidha, kesi nyingi zinazofikishwa polisi zikihusu fumanizi huishia kwa wagoni kuelewana au kulipana fidia lakini wanawake ndiyo wanaathirika zaidi kwani wengi wanaofumaniwa huachika.

 Chanzo:
Haruni Sanchawa na Makongoro Oging'   ( GPL)