JESHI la Polisi mkoani Mbeya limemfukuza kazi askari wake Enock Daffa (22) kwa tuhuma za kufanya mapenzi na mtuhumiwa wa kike mwenye umri wa miaka 25 katika Kituo cha Polisi cha Mji mdogo wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani hapa.
Kwa mujibu
wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, askari huyo
alitenda kosa hilo Novemba 21,2012 na kwamba mtuhumiwa aliyefanya naye
mapenzi alikuwa akikabiliwa na kosa la wizi.
Kamanda Athumani
alisema kuwa mbali ya kufukuzwa kazi askari huyo tayari amefikishwa
katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi ili sheria iweze kuchukua mkondo
wake.
Aidha alisema kuwa hali kama hiyo haitaweza kuvumiliwa na Jeshi la Polisi na kwamba atakayebainika kufanya tukio kama hilo adhabu yake itakuwa ni kufukuzwa kazi.
Kamanda huyo alitoa wito kwa
askari polisi kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za Jeshi la
Polisi kama mwongozo unavyowaagiza ili kulinda maadili ya Jeshi la
Polisi ambacho ndicho chombo kinachotumika na wananchi katika
kuzisimamia sheria.
Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa
askari huyo alisema kuwa kitendo alichofaya mtoto wake si cha kiungwana
ambacho pia kimetia fedheha familia yake pia kwa jeshi la Polisi
ambalo limepewa dhamana ya kutunza usalama wa raia na mali zake.