"WASANII WA COMEDY HAPA NCHINI TUNADHARAULIKA SANA"....MTANGA

WAKATI mataifa makubwa wasanii wa komedi wakiwa wanapewa nafasi kubwa kuliko hata wengine, mchekeshaji wa hapa bongo Hamisi Changare, ‘Mtanga’, amesema kuwa bado kuna haja kubwa ya wadau wa tasnia hiyo waelimishwe juu ya kazi hiyo kwani inaonekana wazi kuwa wanadharaulika pale wanapopewa kazi kwa ujira mdogo kuliko wengine ambao unakuta wanacheza sehemu ndogo lakini wanapewa ujira mkubwa. Kauli ya mchekeshaji huyo inaukweli mkubwa ndani yake kwani wachekeshaji wengi wa hapa nchini wamekuwa wakipewa nafasi kwenye filamu nyingine lakini bado ujira wao unakuwa mdogo huku wakishindwa kuthamiwa kama wasanii wengine wanavyoheshimiwa.

Mtanga ni mmoja ya wachekeshaji wa muda mrefu, ambapo kwa upande wake alisema kuwa dharau wanazopewa hajui ni kwa nini lakini anahisi inatokana na uchekeshaji wao au kuchezaji sehemu ndogo ndogo katika filamu ambazo uhusika wake hauna maana sana.


Alisema kuwa wasanii wengi wa komedi wamekuwa wakicheza kama wafungua geti, au wafanya kazi wa ndani na hiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa washindwe kupewa heshima.


Alisema wasanii wengine wamekuwa wakichukuliwa kwa dau kubwa katika kazi lakini wale wa komedi huwa wanapewa malipo kidogo, kitu ambacho kimekuwa kikiongeza umaskini kwa wasanii wa fani hiyo


Hata hivyo alisema kuwa kuchekesha kunahitaji kipaji cha hali ya juu sana lakini bado wanapofanya kazi nzuri malipo yao yanakuwa madogo, tofauti na wengine ambao hutumia maelekezo mengi kutoka kwa muongozaji.


“Fani yetu imekuwa ngumu sana sijui kwa nini wadau wamekuwa wakitudharau sana, tatizo kubwa lipo kwenye malipo wengi huwa wanashindwa kufanya kazi ya mtu kwa sababu wanacholipwa tofauti na kazi anayofanya hivyo bado tuna nyonywa tena kwa kiasi kikubw sana,” alisema.