.
Moja,
Waheshimiwa Wabunge Halima Mdee, Joshua Nassari, Kangi Lugola, Esther
Bulaya, Deo Filikunjombe, Raya Ibrahim, Amina Mwidau na David Kafulila
walihudhuria tamasha la vijana wa Kigoma All Stars kwa kualikwa na
Mratibu wa kundi hilo Mwasiti Almasi.
Wabunge
wengine walialikwa lakini hawakutokea wakiwemo Joseph Mbilinyi, David
Silinde, Amos Makala, Vicky Kamata na Peter Serukamba. Wabunge hawa
hawakualikwa na mimi bali nilisaidia 'logistics' tu. Lengo la
kushauriana na Vijana wa Kigoma All Stars kuwaalika wabunge kutoka vyama
mbalimbali lilikuwa ni kuonyesha umoja na mshikamano wa nchi bila
kujali vyama vya siasa.
Wabunge
wote walioalikwa waliambiwa hii ni shughuli ya muziki na wala
sikufanya mazungumzo nao yeyote ya awali au kuwaambia au kukubaliana
nini cha kuzungumza au hapana. Tamasha lilikuwa la muziki na
halikuhusika kabisa na siasa. Ni bahati mbaya sana kuwa kuna matamshi
ya kisiasa yalitamkwa katika shughuli ile.
Waheshimiwa
wote walipewa nafasi ya kusalimia na wote walizungumza. Wabunge
waliozungumza kwa muda mrefu kidogo ni ndugu Halima Mdee, Joshua
Nassari, Deo Filikunjombe na Kangi Lugola. Hotuba
za Wabunge wote zilirekodiwa kwenye video neno kwa neno na video hizo
zitawekwa wazi kwenye blogu yangu kama sehemu ya documentary ya tamasha
lile la kihistoria.
Pili,
sikuhusika kwa namna yeyote ile na kuandikwa kwa habari hii iliyozusha
mjadala. Wala sikujua kama habari hii ingeandikwa maana katika ziara
ile sikuita mwandishi hata mmoja maana nilitaka liwe tukio la Kigoma
tu. Mimi kama mlezi wa KigomaAllStars na vijana wenyewe tulijikita
katika 'shukrani Kigoma' kwa watu wa Kigoma.
Kama
mwandishi kaandika ambayo wabunge hawa hawakuyasema basi itaonekana
kwenye videos hizo. Wabunge wenyewe wanajua kwenye nafsi zao nini
walisema Kigoma na kipi kiliwasukuma kusema walioyasema Kigoma.
Nisingependa
kuhusishwa kwa njia yeyote ile na matamshi yao, habari iliyowanukuu na
hata makanusho yao. Maana mwisho wa siku ukweli ndio utasimama. Suala
la Urais lisitupotezee muda kwani kuna mambo mengi sana ya kujadili
kuhusu nchi yetu. Taharuki ambazo watu wanazipata masuala ya urais
yanapotajwa zinashangaza sana.
Chama
changu bado hakijatangaza rasmi mchakato wa kupata mgombea Urais. Hivi
sasa chama hakina mgombea Urais mpaka hapo mchakato utakapotangazwa
ambapo wanachama wataruhusiwa kuomba kupeperusha bendera ya chama.
Mwanachama wa chama chetu atakaye kubalika na jamii na wajumbe wa
mkutano wa uteuzi ndiye atakuwa mgombea wetu. Kwa sasa hayupo na hivyo
tusipoteze muda kujadili jambo hili.
Mzee
Thabiti Kombo alituachia usia tunapokuwa tunazungumza. Alisema 'weka
akiba' sio akiba ya fedha, bali ya akiba ya maneno. Tuweke akiba ya
maneno. Tusimalize yote.