Msemaji Mkuu wa kambi ya Upinzani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imefichua ufisadi mkubwa wa mamilioni ya
dola za Marekani zinazodaiwa kutaka kuibwa kupitia mkataba wa siri
uliofikiwa baina ya kampuni moja ya uwindaji ya Kitanzania na kampuni
mbili za kigeni kwa ajili ya kufanya utafiti wa uchimbaji wa madini ya
urani kinyume cha sheria ya matumizi ya ardhi.Kampuni hiyo ya uwindaji imetajwa kwa jina la Game Frontiers of Tanzania
Limited inayomilikiwa na Mohsin M. Abdallah na Nargis M. Abdallah.Kampuni hiyo inadaiwa kuingia mkataba na kampuni za Uranium Resources PLC na Western Metals Limited, kwa ajili ya kazi hiyo, katika kijiji cha Mbarang’andu, kilichoko katika wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Ufisadi huo uliibuliwa na Msemaji Mkuu wa kambi hiyo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, wakati akiwasilisha hotuba yake kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2012/13, bungeni jana iliyokuwa imewasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Kwa mujibu wa Mdee, mkataba huo ulitengenezwa na kampuni ya wanasheria ya Kitanzania ya Rex Attorneys na kwamba, ulisainiwa Machi 23, 2007, huku vipengele vyake vikiainisha kwamba, unatakiwa uwe wa siri.
Mdee alisema kwa mujibu wa mkataba huo, malipo yaliyoafikiwa baina ya kampuni hizo kwa kazi hiyo ni ya dola za Marekani milioni sita (sawa na Sh. bilioni 9.6), ambazo zitalipwa kwa awamu mbili.
Kwa mujibu wa Mdee, malipo ya kwanza, yatafanyika pale uzalishaji wa urani utakapoanza.
Alisema malipo mengine ni ya dola za Marekani 250,000 (Sh. milioni 400), ambayo kampuni hizo zimekubaliana ni ya baada ya kampuni za madini kukamilisha utafiti wa urani na kupata kibali cha uchimbaji.
Malipo mengine alisema ni ya dola za Marekani 55,000 (Sh. milioni 88) kila mwaka kama fidia ya kushindwa kufanya biashara na usumbufu unaotokana na shughuli za machimbo kwenye kitalu na kwamba malipo hayo yatafanyika kila Machi 31.
Mengine ni ya dola za Marekani 10,000 (Sh. milioni 16) kwa vijiji vitakavyoathiriwa na utafiti wa urani.
Hata hivyo, Mdee, alisema wakati kampuni hiyo ya uwindaji ikiingia mkataba huo wa siri, sheria ya zamani ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 1974 na sheria mpya namba 5 ya mwaka 2009 zinamruhusu mtu aliye na leseni ya uwindaji kuwinda wanyama tu na siyo vinginevyo.
Alisema pia sheria namba 4 ya ardhi ya mwaka 1999 na sheria namba 5 ya ardhi ya vijiji ya mwaka huo, zinatamka bayana kwamba ardhi inajumuisha vitu vyote vilivyo juu ya ardhi na chini ya ardhi isipokuwa madini au mafuta.
“Na kwa mujibu wa sheria za Tanzania linapokuja suala la madini, umiliki unatoka kwa mtu binafsi na kurudi serikalini. “Na ni serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ndiyo pekee yenye mamlaka ya kutoa leseni ya kutafuta madini kwa kampuni za madini,” alisema Mdee.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka serikali kueleza uhalali wa mkataba baina kampuni hizo na kueleza sheria inayoipa kampuni ya uwindaji haki ya kualika kampuni ya nje kwenye eneo ambalo haina umiliki kufanya utafiti na hatimaye kuchimba madini hatari ya urani.
Pia aliitaka serikali kueleza nini mustakabali wa Watanzania wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka mbuga hiyo, ambao wanaishi maisha yao ya kila siku pasipo kujua kama kuna utafiti wa madini hatari ya urani unaoendeshwa kwa siri kubwa.
“Ni serikali gani yenye uwakilishi mpaka ngazi ya kitongoji na usalama wa taifa mpaka ngazi ya chini kabisa za utawala inashindwa kuyaona haya?” alihoji Mdee.
Pia aliitaka serikali kuangalia hatua za kuchukua dhidi ya wawekezaji katika mashamba 13 walioshindwa kuyaendeleza kwa asilimia 100, pamoja na wawekezaji katika mashamba 14 walioshindwa kabisa kuendeleza mashamba waliyonunua.
Alitoa mfano kwa mwekezaji anayejiita Chavda Group aliuziwa mashamba saba yenye ukubwa wa hekta 25,000 kwa bei ya kutupa katika maeneo tofauti nchini, ambapo kikubwa alichokifanya ni kutumia hati za shamba kuchukulia mikopo kisha kuyatekeleza.
“Hivi kweli unahitaji kuwa na akili nyingi kuyaona haya? Nyuma ya Chavda Group wako kina nani?” alihoji Mdee na kuongeza:
“Ni familia hii hii ya Chavda (V.G. Chavda na kaka yake P.G. Chavda) waliojitwalia mkopo wa dola za Marekani milioni 3.5 mwaka 1993 chini ya DCP (Dept Conversion Program) wakiahidi kufufua mashamba ya mkonge Tanga ndani ya miaka 10 na kupata dola za Marekani milioni 42.
“Walipopata mapesa hawakufanya lolote na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi yao. Kwa utaratibu huu, lazima tuwachukulie wawekezaji wa aina hii kama ni ‘waporaji’ na hawana tofauti na majambazi yanayoiba benki kwa kutumia nguvu.”
Aliitaka serikali kupitia wizara hiyo kusimamia sekta ya ardhi kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo hayajaendelezwa na wawekezaji yanarejeshwa serikalini bure bila fidia kwa ajili ya kutafuta wawekezaji wengine wenye mtaji wa kutosha watakaoyaendeleza mashamba hayo.
Alisema kwa mashamba ambayo tayari yana wakulima wadogo wadogo wanaoendesha shughuli zao za kilimo, serikali ipange utaratibu wa kuwamilikisha maeneo husika ili kuondokana na dhana ya ‘uvamizi’ au kukodishwa ardhi kwa ajili ya kilimo.
Mdee alisema zoezi hilo lazima lifanywe kwa uwazi ili kuepuka udanganyifu uliotokea katika maeneo mengine nchini, ambapo vigogo na watu wenye nafasi zao walijitwalia ardhi wakijifanya na wao ni sehemu ya wanakijiji.
MATUMIZI YA ZIADA
Alisema kwa miaka miwili mfululizo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuwa ikitumia fungu la mshahara kuliko kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.
Mdee alisema kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2010/2011, wizara hiyo iliidhinishiwa Sh. bilioni 6.4 kwa ajili ya mishahara, lakini katika kipindi cha Julai 2010 hadi Mei 2011 ilitumia Sh. bilioni 8.4 kulipa mishahara.
Alisema pia katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 wizara iliidhinishiwa Sh. bilioni 7.5 kwa ajili ya matumizi ya mishahara, hadi Mei, mwaka huu kiasi cha Sh. bilioni 9.7 zilitumikia kulipa mishahara.
Kutokana na hilo, aliitaka serikali kueleza tofauti hiyo ya zaidi ya Sh. bilioni 2 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge na kiasi kilichotumiwa na wizara kwa miaka miwili mfululizo imetokana na nini.
Pia alisema katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 na 2011/2012, Sh. milioni 431.5 na Sh. milioni 171.9, zilitumika kuandaa andiko la kuomba eneo la nyongeza nje ya ukanda wa kiuchumi baharini, hivyo akaitaka serikali kutoa mchanganuo wa matumizi husika na kuainisha ni kwa namna gani andiko limeweza kuigharimu serikali zaidi ya Sh. milioni 600.
MRADI WA KIGAMBONI BATILI
Wakati huo huo, Mbunge wa Kigamboni (CCM), Faustine Ndugulile, amegeuka mbogo bungeni na kusema mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni ni batili kwani umekiuka sheria na kwamba, kinachofanywa na serikali ni kung’ang’ania udalali kwa kutaka kuchukua ardhi ya wananchi maskini na kuiuza kwa bei kubwa kwa matajiri, kinyume cha ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema kitendo hicho kinasikitisha na kwa hiyo, kama serikali ilichukua fedha za mwekezaji kwa ajili ya kumuuzia maeneo ya wananchi wa Kigamboni, basi imemrudishie na kumweleza “Kigamboni kimenuka.”
Dk. Ndugulile alisema sheria ya ardhi inasema kwamba, ardhi ni mali na kwamba, mwananchi anapaswa kunufaika na ardhi yake na kumtaka Waziri Tibaijuka aeleze kama ni sera ya serikali kudhulumu ardhi ya maskini na kuwapa matajiri na nini maana ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Alisema mpango wote wa kuanzisha mradi wa Kigamboni una upungufu mkubwa wa kisheria, kwani ulitangazwa kupitia Gazeti la Serikali namba 229 la Oktoba 24, 2008 kupitia kifungu namba 34 cha sheria ya utoaji ardhi namba 47 ya mwaka 1967.
Hata hivyo, alisema wakubwa wamekuwa na papara, kwani sheria hiyo kwa mujibu wa kifungu namba 8 (3) (A), kinataka kabla ya kuanza mchakato, lazima ufanyike mkutano wa hadhara katika eneo husika na wananchi watoe ridhaa, lakini mkutano huo haujawahi kufanyika.
“Mheshimiwa waziri atuambie hapa, ni lini mkutano huo ulifanyika, na wapi na wananchi gani wa Kigamboni walioshiriki?” alihoji Dk. Ndugulile.
Dk. Ndugulile alisema kauli ya waziri kwamba, mpango wa kuanzisha mradi huo umekamilika haina ukweli.
Alisema kuhusu kauli ya waziri kwamba, ana asilimia 10 ya fedha za uendeshaji wa mradi huo, wakati katika bajeti ya mwaka jana, wananchi waliwapa muda hadi Juni 30 wawe wametekeleza mradi, lakini mpaka sasa utekelezaji haujaanza.
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya, alisema kuna haja ya serikali kukaa na wananchi wa Kigamboni kuona namna gani wataliweka sawa tatizo hilo.