YANGA YAMPA MBELGIJI MKATABA WA MIAKA MIWILI.

Tom Saintfiet.
KOCHA mpya wa timu ya soka ya Yanga, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji amesaini mkataba wa miaka miwili ambao anaweza kuongezwa kama ataipa mafanikio timu hiyo yenye maskani yake katika mtaa wa Twiga na Jangwani. Akihojiwa katika hafla ya kutiliana saini mkataba huyo Saintfiet amesema kazi yake kubwa aliyonayo ni kuhakikisha timu hiyo inatetea ubingwa wake wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza baadae mwezi huu. Kocha huyo ameendelea kusema kuwa anataka kuifanya Yanga mbali na kupata mafanikio katika ligi ya nyumbani lakini pia iweze kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuwa tishio kwa vilabu vingine vya Afrika kama ilivyo kwa klabu ya TP Mazembe na klabu nyinginezo. Amesema kitu cha msingi kwa sasa ni mashabiki pamoja na viongozi wa klabu hiyo kumpa ushirikiano ili kwa pamoja waweze kujenga kikosi imara na chenye ushindani katika kipindi ambacho atakuwa kocha kwenye klabu hiyo.