Na: Majuto Omary, MWANANCHI
KIUNGO
wa Simba, Haruna Moshi ameomba radhi kwa kumchezea rafu beki wa Yanga,
Kelvin Yondani itakayomfanya akae nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki mbili.
Moshi alimkanyaga Yondani juu ya goti kwenye mchezo wa Ligi Kuu
uliozikutanisha Yanga na Simba Jumatano usiku na kumalizika kwa sare 1-1
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza
na Mwananchi, Moshi maarufu kwa jina la 'Boban' alisema kuwa anajisikia
vibaya sana kwani hakudhamiria na kilichotokea ni bahati mbaya.
Boban alisema kuwa Yondani ni rafiki yake wa karibu sana na kilichotokea
hata yeye hakujua matokeo yake.
ìMimi nimekosea, lakini sikujua kwani ule mpira ulikuwa fifty fiftyí,
nilikuwa nauwahi na Yondani alikuwa anauwahi ili kuokoa, matokeo yake
ndiyo hayo, nilivyoosha mguu ili kuuchukua mpira, bahati mbaya Yondani
naye akawa amefika, nasikitika sana kwa yale yaliyotokea,î alisema
Moshi.
Alisema
kuwa baada ya Yondani kutolewa nje na kushindwa kuendelea na mchezo,
alijutia kile kilichotokea na hasa ukaribu wake na mchezaji huyo kwa
miaka mingi, tangu akiwa Simba na sasa baada ya kuhamia Yanga.
ìNaomba radhi kwa Yondani, familia yake, wachezaji wa Yanga, viongozi wa
timu hiyo, benchi la ufundi na wadau wa soka kwa ujumla, sikujua
nilichokifanya kwani nilikuwa katika majukumu ya klabu wala sikutegemea
kitu kama kile kutokea,î alisema Moshi kwa masikitiko makubwa.
Alisema kuwa atajitahidi kukutana na Yondani ili kumjulia hali yake
kwani mbali ya upinzani wa uwanjani, wao ni marafiki wa siku nyingi
sana.
Boban aliwaomba mashabiki wa Yanga wasichukulie tofauti suala hilo kwani
hata yeye mpaka sasa linamuumiza sana.
Naye
Daktari wa Yanga, Juma Sufiani alisema kuwa Yondani amepata ufa
(fracture) katika mfupa wake wa mguu wa kulia na kuchana ligament, hali
ambayo imemfanya awe katika hali mbaya na atakaa nje kwa muda wa wiki
mbili bila ya kufanya mazoezi.
Sufiani alisema kuwa muda wa wiki mbili ni wa muda wa awali tu, lakini
kwa hali ilivyo, inawezekana kabisa akaongezewa muda kutokana na kasi
yake ya kupata nafuu.
Alisema kuwa pamoja na kukaa nje, pia anahitaji kupata uangalizi wa
karibu sana na ushauri huo umetolewa na madaktari wa Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili.
Ni
pigo na anahitaji uangalizi wa karibu sana, kwa sababu rafu ilikuwa
mbaya, lakini ni hali ya kawaida kwa wachezaji, hajavunjika ila maumivu
yake ni sawa na mtu aliyevunjika, kupata fracture na kuchana ëligamentí
ni kati ya magonjwa makubwa sana katika mpira wa miguu,î alisema
Sufiani.
Wakati huohuo; Jumla ya mashabiki 50,455 walishuhudia pambano hilo na
kuingiza sh 390,568,000, huku Yanga na Simba kila moja ikiambulia sh
93.3 milioni.
Watazamaji
50,455 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa usiku kwa
viingilio vya sh 5,000, sh 7,000, sh 10,000, sh 15,000, sh 20,000 na sh
30,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh 93,345,549.15 wakati Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh 59,578,169.49.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni posho ya msimamizi wa kituo sh 240,000,
kamishna wa mechi sh 250,000, waamuzi sh 591,000, mwamuzi wa akiba
(reserve referee) sh 70,000, usafi na ulinzi wa uwanja sh 2,350,000 na
Wachina (stadium technical support) sh 2,000,000.
Umeme sh 750,000, maandalizi ya uwanja (pitch preparation) sh 400,000,
ulinzi wa mechi sh 5,860,000 wakati tiketi ni sh 7,327,000. Gharama za
mchezo sh 31,115,183.05, uwanja sh 31,115,183.05, Kamati ya Ligi sh
31,115,183.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh
18,669,109.83 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
sh 12,446,073.22.
Wakati
huo huo, mechi ya ligi hiyo kati ya African Lyon na Toto Africans
iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex ilishuhudiwa na mashabiki tisa kwa
kiingilio cha sh 3,000 na kuingiza sh 27,000.
Mgawo wa mechi hiyo ulikuwa VAT sh 4,118.6 wakati kila timu ilipata sh
6,864.3. Uwanja sh 2,288.1, gharama za mchezo sh 2,288.1, Kamati ya Ligi
sh 2,288.1, FDF sh 1,372.8 na DRFA sh 915.2.