Wakati ambapo show za Bongo Star Search zinazooneshwa kupitia kituo cha ITV zina wiki tatu tu tangu zianze, mikosi imeanza kumwandama mwanzilishi wa show hiyo, Rita Paulsen.
Siku ya Ijumaa mwandishi wetu alikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia moshi mzito ukitanda maeneo ya Mbezi Beach katika barabara ya Old Bagamoyo mida ya saa mbili asubuhi.
Katika barabara hiyo ambayo huwa na msongamano mkubwa wa magari hususan asubuhi kutokana na wafanyakazi wengi kuwa kwenye harakati za kuingia makazini, iliyapa tabu magari mawili ya zimamoto yaliyokuwa yakijaribu kishindana na msongamano huo wa magari kuwahi tukio hilo la moto.
Haikuwa rahisi kusimama na kujaribu kwenda kwenye eneo hilo ili kujua ni nyumba gani iliyokuwa ikiteketea kwa moto, lakini muonekano wa moshi huo mzito, ulimpa jibu mwandishi huyu kuwa moto uliokuwa unawaka ulikuwa mkubwa.
Bahati mbaya kama ilivyo katika matukio mengi ya moto, watu wa zima moto walifika wakiwa wamechelewa na kukuta moto uliokuwa ukiwaka kwa hasira, umeteketeza mali nyingi zilizokuwa ndani na kuiacha nyumba hiyo ambayo tulikuja kufahamu baadaye kuwa ni ofisi za Benchmark Productions, ikiwa imebaki kama gofu la nyumba iliyopigwa na mabomu enzi za vita vya pili vya dunia.
Benchmark Productions ni kampuni ya Rita Paulsen ambayo huandaa vipindi vya Bongo Star Search.
Japo ni tukio baya, timing yake haikuwa mbaya kwakuwa tayari mizunguko ya usaili wa show hiyo ilikuwa imekamilika,lasivyo ingeziathiri kiasi cha kuzisitisha kwa muda ili kumpa muda Madam Rita apone kidonda chake.
Moto huo uliotokana na shoti ya umeme, umemsababishia hasara kubwa ambayo inafikia shilingi milioni hamsini kwakuwa nyumba hiyo ilikuwa ikitumika kama stoo ya kuhifadhia vifaa vya kazi za utayarishaji za kampuni yake ambavyo vyote viliteketea.
Pamoja na hasara yote hiyo Madam Rita amesema show zake za Bongo Star Search zitaendelea kama kawaida.
Hata hivyo tukio la moto lilitokea baada ya tukio jingine ambapo Rita Paulsen aliibiwa begi lake lililokuwa na vitu vingi vya thamani zikiwemo shilingi milioni tatu pamoja na kadi za benki, vitambulisho na funguo za gari Mercedes Benz ambayo anasema mpaka sasa imebaki kuwa mdoli tu kutokana kuwa na ufunguo mmoja tu.
Wezi hao walilipokonya begi lake wakati alipokuwa amesimama kuzungumza na mtu barabarani.
Katika kipindi cha wiki moja na siku chache tu, Madam Rita amejikuta akila hasara kubwa ambayo itamchukua muda kuiweka sawa. Kama binadamu yeyote, tunaamini mwanamke huyo mjasiriamali atakuwa amevunjika moyo, hivyo ni jambo jema kumwombea kwa Mungu ili mambo yake yakae sawa tena.