Waandishi Wetu, Dar na Dodoma
KADA
mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu
Mstaafu, John Malecela ameitaka Serikali kuchukua hatua kali za
kisheria endapo itathibitika kuwa kuna wabunge wanaojihusisha na
vitendo vya rushwa
Kauli
hiyo ya Malecela mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika nchini, imekuja
kipindi ambacho tuhuma hizo za baadhi ya wabunge kuhongwa zikiwa
zimetikisa Bunge na nchi kwa ujumla.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20
tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu Huria (OUT) jana, Malecela alisema: “Ni
aibu kubwa kwa Bunge kama mhimili wa dola wa kutunga sheria na
kuisimamia Serikali kuhusishwa na rushwa.”
“Wabunge
ndiyo wanatunga sheria ya kupiga vita rushwa sasa inakuwaje na wao
tena wanajihusisha na uozo huo? Ningeshauri hatua kali zichukuliwe
dhidi yao endapo kweli tuhuma hizo zitathibitishwa,” alisema Malecela
na kuongeza:
“Tuhuma
hizi nzito zinaelekea kulichafua Bunge hivyo, kama Spika Anne Makinda
alivyoahidi uchunguzi wa kina ufanyike ili kurudisha imani ya wananchi
dhidi ya viongozi wao.”
Sendeka, Msafiri wanena
Hatua
ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kuwataja
wabunge saba wa CCM kuhusika na tuhuma za ufisadi, zimechafua hali ya
hewa bungeni baada ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka
kuomba mwongozo wa Spika kama anaweza kumshtaki mahakamani kwa madai
kuwa amemdhalilisha.
Wakati
Ole Sendeka akieleza kusudio lake hilo, Mbunge wa Viti Maalumu, Sara
Msafiri ambaye Lissu alimtuhumu kufanya biashara ya matairi na Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco) na kumwomba Katibu Mkuu wa Nishati na
Madini Eliakim Maswi, rushwa ya Sh50 milioni alisema anasubiri matokeo
ya uchunguzi unaofanywa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge.
Ole
Sendeka na Msafiri ni miongoni mwa wabunge saba wa CCM waliotajwa na
Lissu juzi, kwamba wanalichafua Bunge kutokana na kujihusisha na mambo
yenye mgongano wa kimasilahi
Wabunge
wengine waliotajwa na Lissu ni Nasir Abdallah (Korogwe Mjini), Mariam
Kisangi na Vicky Kamata (Viti Maalumu), Charles Mwijage (Muleba
Kaskazini) na mbunge mmoja ambaye hatutamtaja kwa sababu hajapatikana
kuzungumzia tuhuma zake.
Wabunge
hao wote walishazungumzia tuhuma zaona kukanusha kuhusika. Lakini,
jana Ole Sendeka baada ya kipindi cha maswali na majibu, aliomba
mwongozo wa Spika kutaka ufafanuzi endapo kauli hizo za Lissu zina
kinga ya Bunge ili aende mahakamani na kama hazina alitaka mwongozo wa
Spika.
“Mheshimiwa
Spika, jana Lissu aliitisha mkutano na waandishi wa habari na
akanitaja mimi na wabunge wengine wa CCM kwamba ndiyo tunaohusika na
tuhuma hizi za ufisadi. Sasa naomba mwongozo wako. Kauli hizo zina
kinga ya Bunge au la ili niweze kwenda mahakamani,” alisema.
Katika mwongozo wake, Spika Makinda alisema kwa kuwa kauli hizo zilitolewa ndani ya maeneo ya Bunge zina kinga...
“Ila
napenda kuwaambia kuwa Bunge hili liwe na subira. Kuhusu aliyoyasema
jana Lissu sisi tutamtaka yeye ndiye awe shahidi wa kwanza katika vikao
vya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge. Atupe ushahidi tupate
pa kuanzia.”
Kwa
upande wake, Msafiri alisema ana imani kwamba kamati husika itatenda
haki na kwamba yeyote anayemtuhumu apeleke ushahidi katika kamati hiyo.
"Siwezi
kuzungumza kitu kwa sasa maana tuhuma ni tuhuma tu, mara huyu kasema
hili mwingine kasema lile, kwa hiyo tusubiri tu matokeo ya Kamati ya
Bunge na tumeambiwa inafanya kazi kwa kasi sana,” alisema Msafiri.
Msafiri pia anadaiwa kwenda kwa Maswi kumwomba radhi na kumsihi asitoe ushahidi dhidi yake mbele ya Kamati ya Bunge.
Habari
kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini zimedai
kuwa baada ya mjadala wa ufisadi kulipuka bungeni mwishoni mwa juma,
mbunge huyo aliamua kuomba radhi kama njia ya kujinusuru na adhabu
inayoweza kutolewa dhidi yake kama Bunge litathibitisha kuwa aliomba
rushwa.
Sheria
ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge namba 3 ya mwaka 1988, inataka
Mbunge anayethibitika kutumika na watu kutoa michango au kuandika
bungeni kwa masilahi ya mtu huyo ama kujihusisha mwenyewe katika
masuala ya rushwa, afukuzwe ubunge na kufungwa kifungo cha miaka
mitano.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, mbunge huyo anadaiwa kufika Ofisi za Nishati
na Madini zilizoko Mjini Dodoma Jumapili asubuhi, ikiwa ni siku moja
baada ya Bunge kupitisha azma hiyo. Akaonana na Maswi na kuomba radhi
katika kikao kilichowashirikisha watu watatu.
Habari
zaidi zimeeleza kuwa lengo la mbunge huyo kuomba radhi ni kumshawishi
katibu huyo ili asishirikiane na mamlaka zinazofuatilia tuhuma hizo
ikiwamo Bunge katika kutoa taarifa kuhusu suala hilo.
Kuhusu suala hilo, Msafiri pia alisema anaiachia Kamati hiyo ya Bunge kufanya kazi yake.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipotakiwa kuzungumzia
hatua ya mbunge huyo kuomba radhi, alisema asingependa kuzungumzia
masuala ya watu, bali utendaji wa kazi katika wizara yake.
Hata
hivyo alieleza kuwa anachofahamu siku ya Jumapili, katika Ofisi za
Wizara ya Nishati na Madini Dodoma, kulikuwa na kazi ya watendaji wa
wizara hiyo kuonana na wabunge.
Nape aitega Chadema
Katika
kile kinachoonyesha ni kuchukizwa na tuhuma hizo, CCM kimetoa tamko la
kulaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa
kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa
zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza
na waandishi a habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye alisema zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya
siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya
wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
“Mfano
mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu ambaye ni Mbunge wa
Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni cha kutoa
aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na Tanesco
na kwamba, ndiyo watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa,” alisema Nape na
kuongeza:
“Cha
kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote
tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa
Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa
hii.”
Nape
alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zina lengo la kuuficha ukweli
na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
Alisema
CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapowahusisha viongozi ambao
wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwani vinavuruga uchumi wa nchi na kwamba
haitoshi kuwaita wala rushwa tu, bali ni zaidi ya wahujumu uchumi...
“Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa
hili na iwe fundisho kwa wengine,” alisema Nape.
Nape
alisema CCM kinawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na
Madini wakiongozwa na Waziri wao, Profesa Sospeter Muhongo, Manaibu
wake, Stephen Massele na George Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa
uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi
waliokaa kwenye wizara hiyo.
“Tunaamini
uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii utaigwa na watumishi
wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za
nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania
yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao,” alisema Nape.