Mitaala Shule Za Msingi Inawachanganya Wanafunzi – Walimu

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, akizungumza na mtandao wa Thehabari.hivi karibuni.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitopeni kutoka Wilaya ya Korogwe.

“Mabadiliko ya mitaala na mchanganyiko wa vitabu bila utaratibu mahususi ni tatizo, kwa sasa hivi kila shule ina kitabu chake katika somo fulani…hata hivyo licha ya mabadiliko ya mara kwa mara hakuna maandalizi, mimi tangu nimalize chuo 1979 sijaenda semina yoyote wala mafunzo kujiandaa na mabadiliko ya mitaala hii. Hili linachangia pia,” alisema mwalimu Mtui.

Akifafanua zaidi Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Muungano, ya wilayani Moshi, Ashati Elihaki alisema mbali na mchanganyiko juu ya suala la vitabu vya masomo mabadiliko ya mitaala yamegeuza baadhi ya masomo kubaki kama ‘kiini macho’ jambo ambalo ni tatizo kwa walimu.

“…angalia kwa mfano somo kama la Tehama linaloanza kufundishwa darasa la tatu hadi la saba somo hili lipo kinadharia zaidi, hakuna walimu ambao wameandaliwa kufundisha somo hili lakini linatakiwa kufundishwa eti kwa kutumia mwongozo wa mwalimu kimsingi hii si sawa,” alisema Elihaki.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitopeni ya Mjini Korogwe, Theodolph Karigita alisema tofauti na ilivyokuwa hapo awali mitaala ya sasa imevurugwa kiasi kikubwa jambo ambalo linawachanganya walimu na hata wanafunzi hivyo kushindwa kufanya vizuri.

“…Mitaala imevurugwa sana, kunamchanganyiko wa masomo nadhani unakumbuka kuna kipindi baadhi ya masomo yaliunganishwa kama Jiografia, Historia na Uraia wakaita maarifa ya jamii…kipindi hiki wanafunzi walifanya vibaya sana hivyo ikabadilishwa sasa watoto wanafanya vizuri tofauti na awali,” alisema Karigita.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lwengera Darajani, Youze Mbwambo alisema idadi kubwa ya masomo kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la tatu ni chanzo kingine cha wanafunzi hao kufanya vibaya kwani wamekuwa wakibebeshwa mzigo pasipo sababu za msingi.

Akizungumzia hoja hizo zilizotolewa na baadhi ya walimu, Ofisa Elimu Taaluma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Elius Mkwizu alisema mabadiliko yanayofanywa na wataalamu hufanywa kwa malengo mazuri licha ya kuwepo na changamoto kadhaa maeneo tofauti.

Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Taasisi ya HakiElimu.