CHANZO KINATIRIRIKA
“Watu walisema eti Wema na Wolper wamepatana kinafiki, sasa ngoja niwape mchongo...wapo hotelini (akiitaja hoteli yenyewe lakini tunaificha jina kwa sababu maalum) tena katika chumba kimoja.
“Hawana uadui wale tena, sasa aibu itabaki kwa wale wanaowagombanisha na kupeleka umbeya kila upande,” kilidadavua chanzo hicho kwa sharti la kutochorwa jina lake gazetini.
TIMU YA RISASI MZIGONI
Bila kupoteza muda, ‘wazee wa kazi’ walichukua vitendea kazi vyao na kukimbilia katika hoteli waliyoelekezwa ambapo kweli walifanikiwa kuwakuta Wema na Wolper wakijiachia kwa raha zao.
Hawakuonesha mshtuko, wala kuzuia waandishi wetu wasiwafotoe picha, badala yake ndiyo kwanza waliweka na pozi.
SHUKA MOJA, KITANDA KIMOJA
Wakiwa na nyuso zenye matabasamu ya nguvu, Wema na Wolper walikuwa wamelala katika kitanda kimoja na kujifunika shuka moja huku wakiendelea na stori za hapa na pale.
Kwa namna ilivyokuwa ni kama hapakuwahi kutokea bifu lolote kati yao.
Waandishi wetu walifanikiwa kuzungumza nao juu ya tofauti zao na hali ilivyo hivi sasa baada ya kuweka mambo sawa.
WEMA ANATOA YA MOYONI
“Nina furaha sana kiukweli, tangu tumemaliza pambano letu pale Taifa (Uwanja wa Taifa) tumekuwa kwenye upendo na amani kama zamani.
“Unajua hakuna maana ya kuwa na bifu...sisi bado ni vijana na tunahangaika kusaka maisha, kwa nini tudumu kwenye bifu? Wolper ni rafiki yangu na yote yaliyopita tumeshayasahau.”
Wema alipopewa nafasi aeleze chanzo cha bifu lao, alisema: “Hayo yameshapita, siwezi kuyazungumzia tena, ninachojua ni kwamba tumepatana na tumefungua ukurasa mpya.”
KUTOKA KINYWANI MWA WOLPER
“Siwezi kusema nilikuwa na ugomvi na Wema, zile ni changamoto tu na kwa sasa zimeisha, sina la kuongeza. Nadhani sasa mtupishe tuendelee na mapumziko yetu.”
RAFIKI WA WOLPER ADUWAA
Shostito wa karibu na Wolper ambaye hakutaka jina lake lichorwe gazetini, alisema hakutegemea kama tofauti kati ya shogaye na Wema zingeisha.
“Nimeamini hakuna rafiki wa kudumu na pia hakuna adui wa kudumu duniani, maana nilikuwa nina shida na Wolper akanimbia nimfuate hotelini, nilipokwenda nikashangaa kumkuta na Wema,” alisema.
KALAMU YA MHARIRI
Kukosea ni sehemu ya ukamilifu wa binadamu, kama Wema na Wolper mmegundua makosa yenu kila mmoja kwa wakati wake anapaswa kujua thamani ya urafiki wake kwa mwenzake na kuanza ukurasa mpya wa kweli.
Bifu halina maana kwa wasanii, mkiendelea kuwa katika umoja, bila shaka mtapiga hatua katika sanaa yenu.