SIJAOMBA FEDHA ZAIDI - RONALDO.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid ya Hispania Cristiano Ronaldo amesema kuwa kukosa kwake furaha katika klabu hiyo hakuhusiani na mambo ya fedha kama baadhi ya vyombo vya habari vinavyosema kwani kikubwa anachotaka yeye ni mkataba wenye faida zaidi. Mshambuliaji huyo ghali zaidi duniani alitawala vyombo vya habari baada ya ushindi wa timu yake wa mabao 3-0 dhidi ya Granada Jumapili iliyopita wakati alipokataa kushangilia mabao mawili aliyofunga katika mchezo huo na baadae kusema kuwa alikuwa na huzuni. Ronaldo aliandika ujumbe katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kuwa kuonyesha uzuni aliyokuwa nayo kumezua mjadala mkubwa huku watu wakimtuhumu kuwa anahitaji pesa zaidi lakini siku moja watu hao watakuja kuona kwamba huzuni yake haihusiana na suala la kuongezwa fedha. Kuna taarifa pia zilizochapishwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa mchezaji huyo alifanya mkutano na rais wa klabu hiyo Florentino Perez Jumamosi na kumwambia kuwa hadhani kama anapewa ushirikiano katika vyumba vya kubadilishia nguo, hana furaha na anataka kuondoka klabuni hapo. Ronaldo ambaye ni mojawapo ya wachezaji wanaolipwa zaidi duniani akikinga kiasi cha dola milioni 13 kwa mwaka, alikana tetesi zote hizo na kuwahakikishia mashabiki wa Madrid kwamba bado ana nia ya kubakia hapo na kushinda mataji zaidi.