US OPEN: SERENA ATINGA ROBO FAINALI KWA KISHINDO.

MCHEZAJI nyota wa tenisi kutoka Marekani, Serena Williams amefanikiwa kutinga robo fainali ya michuano ya wazi ya Marekani baada ya kumsambaratisha Andrea Hlavackova kwa 6-0 6-0. Serena ambaye ni bingwa mara tatu wa michuano hiyo atapambana na Ana Ivanovic aliyemfunga Tsvetana Pironkova kwa 6-0 6-4 katika mzunguko wa nne. Katika mchezo wa wawili wawili Serena na dada yake Venus Williams walishindwa kutamba mbele ya Maria Kirilenko na Nadia Petrova kutoka Urusi baada ya kufungwa kwa seti 2-0 za 6-1 6-4. Kwa upande wa wanaume Andy Murray wa Uingereza alifanikiwa kutinga katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kumfunga Milos Raonic kwa 6-4 6-4 6-2.