VAN PERSIE MAJERUHI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya Manchester United, Robin van Persie alitolewa nje katika kipindi cha mapumziko baada ya kupata majeruhi nyuma ya paja katika mchezo wa kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Hungary ambapo timu yake ilishinda mabao 4-1. Kocha wa Uholanzi Louis van Gaaal amesema kuwa alimbadilisha mchezaji huyo kwa tahadhari ili asiumie zaidi kwenye mchezo huo ambao mpaka mapumziko walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-1. Mabao ya timu hiyo kwenye mchezo huo yalifungwa na Jeremain Lens aliyefunga bao la kuongoza kabla ya Balazs Dzsudzsak wa Hungary kusawazisha kwa penati lakini Martin Bruno Indi aliongoza bao la pili na kupelekea timu hiyo kwenda mapumziko ikiwa inaongoza. Mabao mengine ya Uholanzi yalifungwa na Lens ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo huo na Klaas-Jan Hunterlaar aliyepigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Hungary na kuihakikishia Uholanzi kuondoka na lama zote tatu. Baadhi ya michezo mingine iliyochezwa jana, Hispania ilifanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Georgia huku Ufaransa wakiibugiza Belarus kwa mabao 3-1 wakati Ujerumani nao wakiendeleza wimbi la ushindi kwa kuisambaratisha Austria mabao 2-1.