Mjumbe
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bw. John Nkolo (aliyesimama) akijitambulisha
kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Magesa Mulongo wakati Wajumbe wa Tume hiyo walipokwenda
kujitambulisha kwake jana jumapili tarehe 18. Novemba, 2012 tayari ya kuanza
kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mkoa huo.
Wajumbe wengine ni Bw. Abubakari Ali, Bw. Ussi Ali na Bi. Mwantumu Malale.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Bi. Mwantumu Malale akizungumza wakati wajumbe wa Tume hiyo
walipokwenda kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo jana
jumapili tarehe 18. Novemba, 2012 tayari kuanza kazi ya ukusanyaji wa maoni ya
wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Magesa
Mulongo.
 Mkuu
wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja
na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mara baada ya wajumbe hao
kujitambulisha kwake jana tarehe 18. Novemba, 2012 tayari kuanza kazi ya
ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo. Kutoka kushoto
ni Bw. Abubakari Ali, Bw. Ussi Ali, Bi. 
Mwantumu Malale (na wa kwanza kulia) Bw. John Nkolo.
Na: Ismail 
Ngayonga,Arusha. 18. Novemba. 
2012
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameihakikishia Tume 
ya Mabadiliko ya Katiba mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa wakati wote wa 
kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya Mkoani 
humo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliyasema hayo (jana jumapili tarehe 18. 
Novemba,2012) wakati wa mkutano wake na Wajumbe wa Tume hiyo waliofika Ofisini 
kwake kwa ajili ya kujitambulisha tayari kuanza awamu ya nne ya kazi ya 
ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya mkoani humo inayoanza leo 
jumatatu tarehe 19. Novemba, 2012.
Kwa mujibu wa Mulongo alisema Ofisi yake imejiandaa 
kikamilifu kwa ajili ya kazi hiyo na hivyo ipo tayari kutoa msaada  
kwa Tume hiyo pale inapohitaji. “Katika Mikoa ambayo Tume imeitembelea 
kazi hii imepita vizuri na sisi tutahakikisha kuwa sifa hiyo na sisi pia 
tunaiendeleza” alisema Mkuu huyo wa Mkoa. 
Aidha Mulongo alisema Tume hiyo imepewa jukumu kubwa la 
kitaifa lenye Baraka za Mhe. Rais na Bunge la Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, 
hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha kuwa anatoa ushirikiano kwa kadri 
inavyowezekana.
Kwa upande wake Mjumbe wa Tume hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti 
wa kundi la Mkoa wa Arusha, Bi. Mwantumu Malale alisema Tume katika imekuwa 
ikitumia njia mbalimbali za kukusanya maoni ya wananchi wakati  wa 
mikutano yake ikiwemo njia ya kuzungumza na kuandika.
“Mbali na wananchi pia Viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge 
nao wamekuwa wakijitokeza kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya, tunawaomba 
wananchi wa mkoa wa Arusha nao pia wajitokeze katika mikutano yetu ili nao 
waweze kutoa maoni yao” alisema Bi. Mwantumu.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo jumatatu tarehe 19. 
Novemba, 2012 inatarajia kuanza awamu ya nne ya kazi ya ukusanyaji maoni ya 
wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mikoa 6 nchini. Mikoa hiyo ni Arusha, Dar es 
Salaam, Mara, Simiyu, Geita na Mkoa wa Mji Magharibi, 
Zanzibar.
Mkoani Arusha Tume hiyo leo jumatatu inatarajia kuanza 
 kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Wilaya ya 
Karatu.
 
