Ndugu
zangu,
Katika sehemu ya kwanza ya
makala hii,nilieleza waziwazi kwamba, sisi binadamu, tunao uwezo wa kujua iwapo
tutakufa tukiwa wenye mafanikio au masikini,na hapa ninazungumzia kuanzia ngazi
ya familia hadi ngazi ya taifa.
Aidha niliishia kwa kusimulia kisa cha kweli cha
bwana mmoja aitwaye Pablo,ambae Siku
moja akiwa kwenye kibarua chake, alimsikia mtoto wa tajiri yake akisema, “Baba haiwezekani, tusikate tamaa ni Lazima
tutaweza, kwani wanaoweza wana mkataba gani na Mungu?, ni lini waliongea na
Mungu na kuhakikishiwa kwamba wangekuja kupata?. Tujipe moyo wa kuweza halafu
tufanye”
Pablo anasema, alipofika nyumbani kauli ile ya
kijana wa miaka 25 ilizunguka sana kwenye kichwa chake. Alianza kujiuliza
maswali. Kwanza alijiuliza kama hawa wenye mafanikio walijua kwamba
wangefanikiwa kwa kupewa taarifa. Alijiambia, ‘Hapana’. Akiwa kwenye kujiuliza
aling’amua jambo moja kwamba hawa waliofanikiwa kimapato hawakuwa na taarifa
kutoka kwa mtu yeyote, bali kutoka ndani mwao.
Ni taarifa ya kujiambia
kwamba wanaweza na hivyo wanapaswa kufanya wakiwa kwenye ari hiyo ya kuweza
bila kujali wanakabiliwa na vikwazo gani. Taarifa ya kama mtu atafanikiwa
hujipa mwenyewe kwa kuamini kwamba atafanikiwa. Aliwaza kwamba hakuna hata
mmoja anayeambiwa na yeyote kwamba fanya hadi wakati Fulani na hapo
utafanikiwa, bali watu hujiambia wenyewe kwamba ni Lazima watafanikiwa na hapo
hufanya ili wafanikiwe.
Anasema kuanzia siku hiyo,
alijiambia na kuamini kwamba ni Lazima atafanikiwa. Alifanya shughuli zake
zilezile akiwa na imani hiyo. Anazidi kueleza kwamba, ajabu ni kuwa kuanzia
siku ile alikuwa akifanya shughuli huku
akiwa na hali tofauti kabisa. Alifanya kazi akiiona njia ya kufika mbali, kwa
sababu huko mbali ndiko alikokuwa akikuona ndani ya mawazo na moyo wake.
Kazi zilimwia nyepesi,
upangaji mipango ukajilazimisha kichwani mwake na mabadiliko yakaanza kuonekana.
Kuna wakati huwa tunaogopa kuamini kwamba tunaweza na
tutafika mbali. Siyo kusema au kuwaambia wenzetu, lakini huwa tunaogopa hata
kujiambia wenyewe. Hii inatokana na
malezi na mazingira tulimokulia, inatokana na jamii tunamoishi ambayo inaamini
kwamba mafanikio au mtu kuamini ama kusema atafanikiwa ni kujichulia au
kuringa.
Ndiyo maana kila Mtanzania unayemsalimu atakwambia, ’Hivyohivyo tu.’sisi
ni wahivihivi’ mi mlalahoi’ akina baba kabwela na orodha ni ndefu hapa,ya
majina tunayojipatia kana kwamba ni sifa.
Hatupaswi kuwatangazia wengine kwamba tumefanikiwa au ,
hatupaswi kuwaonyesha au kuwaringia kwamba tumefanikiwa, lakini pia hatupaswi
kuwaonyesha au kuwanyenyekea kwa kuwaambia au kuwaonyesha kwamba tumeshindwa au
tutakwama. Lakini tunatakiwa kwenye fikra zetu tujaze picha(Big the picture) na
kauli za mafanikio, kwenye mioyo yetu tukiri na kujisisitizia kwamba ni Lazima
tutafanikiwa hata kama itachukua miaka mia moja.
Tusidhani
tukifanikiwa tumekosea kama ambavyo siasa ya ujamaa na kujitegemea hapa nchini
ilitafsiriwa vibaya na kutufanya tuamini kwamba mafanikio ni dhambi na aibu kwa
mtu kuwa nayo. Tusidhani kwamba kuamini katika kufanikiwa ni kujichulia
kama baadhi ya mila zetu zilivyotufundisha, ambapo kule vijijini mtu akivuna
mazao mengi sana, wengine huanza kunong’ona kwamba mtu huyo atapata msiba au
mkosi. Tujiambie kwamba tumefanikiwa na
tutafanikiwa zaidi, kwa sababu fanikio
la awali la binadamu ni kujua namna nzuri ya kufikiri au kutumia mawazo yetu.
Kwa hiyo, kama unaamini
kabisa kutoka moyoni mwako au unahisi kwamba wewe huwezi kamwe kufika popote
kimafanikio, ujuwe wazi kwamba hutafika popote, utakufa maskini. Lakini
hujachelewa kwa sababu sasa umelifahamu hilo, unachotakiwa kufanya ni kubadili
hiyo imani yako.
Unabadili kwa kuanza
kuamini kwamba utafanikiwa, kwa sababu mafanikio hayachagui mtu kwa rangi au sura,
umri wala jinsia, bali namna mtu anavyoamini katika mafanikio na kutenda.
Kumbuka hata hivyo kwamba,
hatuzungumzii mafanikio yatokanayo na kuwaumiza wengine au kujiumiza wenyewe.
‘Mafanikio’ yatokanayo na rushwa, magendo, utapeli, ujambazi, ukahaba, ukuadi
na mengine, hayo kamwe siyo mafanikio bali ni vyanzo vya matatizo mengine
maishani mwetu.