Michoro Ya Kampasi Ya Muhimbili Itakayojengwa Mloganzila Kisarawe
Michoro
ya ujenzi wa Kampasi ya Mloganzila iliyo kijijini Kwembe katikati ya
Wilaya za Kisarawe Mkoa wa Pwani na Kinondoni Mkoa wa Dar es salaam. Hii
ni sehemu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili
(MUHAS) inayojengwa kwenye eneo la ekari 3800 kwa ajili ya kutolea
mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari na huduma za Afya wapatao 15,000 kwa
mwaka, na pia itakua sehemu ya kutolea matibabu ya maradhi yote makuu na
ya kawaida nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili, ujenzi wa Hospitali hii, ambayo pesa ya ujenzi wake
imeshapatikana, unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Januari, 2013 na
unatarajiwa kukamilika miaka miwili baada ya ujenzi kuanza. Kwa maneno
mengine Kampasi ya Muhimbili ya Mloganzila inategemewa kuanza kazi
mwanzoni mwa mwaka 2015.
Tayari wataalamu na wafanyakazi wanaotarajiwa kufanya kazi katika
kampasi ya Mloganzila wameshaanza mafunzo ndani na nje ya nchi. Mara
hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itakapokamilika itakua na uwezo wa
vitanda vya kulaza wagonjwa mia sita (600).
Sambamba na kampasi ya MUHAS ya Mloganzila pia ujenzi wa Kampasi ya Afya
ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) umeshaanza na kufikia hatua ya juu na
ambapo pia hospitali hiyo inatarajiwa kuanza shughuli zake rasmi mwaka
2015.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (National Health
Insurance Fund) NHIF Bw. Emmanuel Humba mchakato wa kufanikisha
uanzishaji wa Chuo Hospitali hiyo vimeshaanza ambapo baadhi ya wataalamu
wakiwemo Madaktari na watumishi wengine wako nchini na nje ya nchi kwa
ajili ya masomo na mafunzo mbalimbali.
Chuo hicho kinatarajia kuwa na vifaa vya kisasa vya tiba vinavyokidhi
mahitaji ya Afya na Elimu ya Udaktari wa kiwango cha Kimataifa, ikiwa ni
mikakati kabambe ya serikali ya awamu ya nne katika kuhakikisha nchi
ina wataalamu wengi na huduma za kisasa za afya ili kuondokana na adha
ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
Kwa sasa MUHAS inachukua takriban wanafunzi 2442 wa udaktari na huduma
za afya kwa mwaka. Hivyo ujio wa kampasi ya Afya Mloganzila na Kampasi
ya afya ya UDOM utaharakisha mpango wa serikali wa kupunguza wastani
wa wagonjwa kwa daktari mmoja kwa kiwango kikubwa. Hivi sasa wastani ni
daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000.
Na Michuzi