Aliyejeruhiwa vibaya ametambuliwa kuwa mkazi wa Tegeta, John Paul ambaye baada ya tukio hilo alipelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala na baadaye Muhimbili.Tukio la Tegeta lilitokea wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wananchi waliokuwa wakipinga operesheni ya kuwaondoa katika hifadhi ya barabara katika eneo hilo saa nne asubuhi baada ya wafanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Mwankinga wakiwa na polisi waliyolikamata gari la mkazi mmoja wa eneo hilo.Hali hiyo ilizua ubishi na baadaye vurugu baada ya wakazi hao kutaka gari hilo lisichukuliwe na polisi.
Vurugu hizo ziliwafanya polisi kutumia nguvu kuwatawanya wakazi hao, kazi ambayo hata hivyo, haikuwa rahisi kwani nao walikuwa wakijibu kwa kuwarushia mawe na fimbo, hali iliyodumu kwa saa kadhaa na kufanya eneo hilo kugeuka uwanja wa mapambano kusababisha maduka kufungwa na mali kuharibiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Chales Kenyela alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza kuwa, kijana huyo alijeruhiwa shavuni na kitu ambacho bado hakijafahamika na kupelekwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.
Kamanda Kenyela alisema kuwa, polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na taarifa zaidi zitatolewa baadaye. Alisema awali, wafanyakazi wa kampuni hiyo wakiwa na polisi, walifika eneo hilo na kuanza operesheni ya kuondoa magari.
“Walipokamata gari la mmoja wa wakazi wa eneo hilo wananchi hao walipinga na kuanza kuwafanyia vurugu polisi ambao walijibu mapigo kwa kupiga mabomu ya machozi na kuwatawanya. Kijana huyo alionekana baadaye akiwa amejeruhiwa na kupelekwa Mwananyamala,” alisema. Katibu wa Afya katika Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala alithibitisha kupokewa kwa majeruhi huyo na kudai kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa alijeruhiwa kwa bomu.
Bisakala alisema hali ya majeruhi huyo ilikuwa
mbaya na uongozi wa hospitali ulilazimika kumpeleka Muhimbili kwa
uchunguzi na matibabu zaidi.Mmoja wa mashuhuda wa vurugu hizo ambaye
hakutaka kutaja jina lake alisimulia jinsi eneo hilo lilivyokuwa:
“Polisi wanarusha mabomu na wananchi wanawarushia mawe, ilikuwa tafrani
kubwa hapa.”
Alisema hali hiyo iliwafanya polisi wajibu kwa
kupiga risasi hewani na kufyatua mabomu ya machozi hali iliyozua
taharuki na baada ya watu kutawanyika, kijana huyo alionekana akiwa
ameanguka chini, huku damu zikimvuja.
Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Eligaeshi alithibitisha kufikishwa kwa kijana huyo katika hospitali hiyo akimtaja kwa jina la John Massawe. Alisema alikuwa amejeruhiwa vibaya kichwani.