Na: Nora Damian MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik, ameagiza kuvunjwa kwa msikiti ulioko kwenye eneo la Shule ya Sekondari ya Majani ya Chai, wilayani Ilala, kwa sababu wahusika walishalipwa fidia tangu mwaka 2004.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa kukabidhi msaada wa madawati 90 na viti 180 kwa Shule za Sekondari Majani ya Chai na Ilala, uliotolewa na kampuni ya mafuta ya TSN, Sadiq alisema yeyote aliyejenga ndani ya mipaka ya shule lazima aondoke.
Alisema msikiti huo ulishalipwa fidia na kwamba wahusika wasiitafute ubaya na Serikali kwa sababu hawana uhalali wa kuendelea kuwepo.
“Ibada ni muhimu lakini fanyia mahali ambapo unastahili na si katika eneo la mtu mwingine…tunaleta migogoro ambayo haina sababu,”alisema Sadik.
“Lazima tuheshimu sheria vinginevyo anaweza kuja askofu na yeye akajenga kanisa lake na matokeo yake ni kuvuruga nchi hii kwa kutozingatia sheria,”alisisitiza.