CECAFA YASIFU NIDHAMU KATIKA MICHUANO YA KAGAME.

Baraza la vyama vya soka Afrika mashariki na kati CECAFA limevipongeza vilabu vyote vilivyo fanikiwa kufikia katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kagame ambayo inaendelea nchini Tanzania. Jumla ya timu nane zimefanikiwa kuingia katika hatua hiyo wakiwemo mabingwa watetezi wa kombe Yanga ambao waliongoza katika kundi B kwa kumaliza hatua ya makundi wakiwa wamejikusanyia jumla ya points 6 kufuatia kupata ushindi katika michezo miwili dhidi ya Salaam Wau ya Sudani kusini na ARP ya Rwanda na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Atletico ya Burundi. Timu nyingine ni Simba, URA na Vita Club toka kundi A na Azam na Mafunzo toka kundi C. Katika kundi la B yanga imeungana na APR na Atletico kucheza hatua ya mtoano. Akizungumza hii leo katibu wa CECAFA Nikolaus musonye amesema wao kama CECAFA wameridhishwa na viwango na nidhamu iliyoonyeshwa na timu zote huku akisifu zaidi mchezo wa jana kati ya Simba na Vita ambao ulimalizika kwa nidhamu ya hali ya juu pasi na kuwepo kadi hata moja ya njano wala nyekundu. Katika hatua nyingine CECAFA imefanya marekebisho ya siku katika ratiba ya michuano hiyo kuanzia hatua ya nusu fainali kwa kutenganisha michezo ya hatua hiyo endapo timu mbili kubwa za Tanzania Simba na Yanga endapo zitafanikiwa kuingia katika hatua ya nusu fainali. Musonye amesema endapo timu hizo mbili za Tanzania zenye mashabiki wengi zitafuzu hatua hiyo basi mchezo wa nusu fainali ya kwanza itachezwa jumatano na mchezo wa pili utachezwa alhamisi tofauti na ilivyo sasa ambapo michezo ya nusu fainali yote inaonekana kwenye ratiba kuchezwa siku moja yaani alhamisi. Amesema hili limezingatia hali ya usalama endapo timu moja itaonekana kupoteza mchezo wake. Timu ambazo zimeaga michuano ni Ports ya Djibout, Salaam Wau ya Sudan Kusini na Tusker ya Kenya.