Viwango vipya vya nauli za daladala na mabasi yaendayo mikoani zimeanza kutumika jana, huku wananchi wakizipinga wakidai zinawaumiza zaidi kiuchumi.
Wakati baadhi wakilalamikia kupanda kwa nauli za
dalala katika maeneo yao, baadhi ya wafanyakazi wa mabasi yaendayo
mikoani wameendelea kutoza nauli ya zamani.
Zoezi la kupandisha nauli nchini lililoanza jana
limewagawanya wamiliki wa magari na kufanya baadhi ya safari za mikoani
kupandisha nauli, huku nyingine zikiendelea kuwa kama zamani wakati
nauli za daladala Dar es salaam zikipanda kama ilivyoagizwa.
Hatua hiyo ya kupandisha nauli ilizua tafrani
baina ya makondakta na abiria waliokuwa wakisafiri katika safari
mbalimbali ndani ya jiji, hususan wale waliokuwa hawajui kuwa jana ndiyo
siku ambapo nauli zilitakiwa kupanda.
Mwananchi liliweka kambi katika Kituo Kikuu cha
Mabasi yaendeyo mikoani cha Ubungo tangu saa 12 asubuhi na kushuhudia
baadhi ya abiria wa safari za Arusha na Kilimanjaro wakibishia kiwango
cha juu cha nauli kilichopanda, hali iliyowafanya baadhi ya abiria
kutishia kususia safari.
Hata hivyo, walilazimika kulipia kiwango hicho cha
ziada kutokana na umuhimu wa safari zao japo kwa majibizano na mawakala
wa kukatisha tiketi waliopo kituoni hapo.
Kwa mujibu wa Ofisa wa Chama cha Kutetea Abiria
Tanzania (Chakua), Gervas Rutaguzinda safari za mikoani ambazo
zilipandisha bei ya nauli ni Arusha, Moshi, Mwanza, Bukoba, Musoma na
Kigoma huku nyingine zikiendelea kama zamani.
Alisema awali nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda
Arusha kwa basi la kawaida ilikuwa Sh18,900 lakini jana tiketi zilikuwa
zikiuzwa kwa Sh22,700 ambapo kutokana na ugumu wa kupatikana chenji
abiria walitakiwa kulipa Sh23000.
“Nimewapokea watu watano wa kwenda Mwanza na
wawili wa safari ya Kigoma ambao walileta malalamiko kuwa walishindwa
kusafiri kutokana na kukosa ongezeko la nauli walilokutana nalo” alisema
Rutaguzinda.
Alisema baadhi ya wamiliki wa basi walibainisha
kuwa watapandisha nauli ifikapo mwezi wa sita, lakini kwa sasa
wataendelea na nauli zao za kawaida.
Naye wakala wa kukatisha tiketi kwa safari za
Arusha na Moshi aliyejitambulisha kwa jina moja la Ipiana alisema
ongezeko hilo limeathiri pato lao kwa kuwa katika nauli ya awali alikuwa
akipata Sh2,000 kama kamisheni kwa kila tiketi, lakini kwa jana fedha
zote zlitakiwa kupelekwa kwa mmliki wa basi.
Mwananchi
Mwananchi