LULU MICHAEL AKABILIWA NA WAKATI MGUMU. MTAANI KWATIBUKA NA NDUGU NAO WASHINDWA KUMUELEWA



NYOTA wa sinema Bongo aliyefariki dunia usiku wa Aprili 7, 2012, Steven Charles Kanumba amezikwa juzi kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam huku mpenzi wake, Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayedaiwa kusababisha kifo hicho, akikumbwa na mazito tena.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mazito hayo huenda yakazidi kumpa wakati mgumu Lulu endapo Mungu hatamuepushia.


KUTOKA KWENYE FAMILIA YA MAREHEMU
Habari zinadai kuwa, mpaka siku ya mazishi, ndugu wa marehemu walisita kumuelewa Lulu kufuatia maelezo yake polisi na utata wa kifo cha Kanumba.

“Baadhi ya ndugu wa Kanumba wameshindwa kumwelewa Lulu. Awali walionekana kukubaliana na maelezo yake jinsi hali ilivyotokea mpaka kifo cha marehemu huyo lakini sasa wamegeuka,” kilisema chanzo.

Kikaongeza: Kinachoonekana kwa sasa, kila wakikaa akili zao zinashindwa kubeba na kuhifadhi maelezo ya Lulu ambayo yalianikwa wazi na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Afande Charles Kenyela.

“Afande Kenyela aliweka wazi maelezo ya Lulu, lakini ndani ya familia kumekuwa na maneno maneno f’lani hali inayoonesha kuwa, ndugu hao wanashindwa kuweka kichwani maneno hayo,” kilisema chanzo.

KAULI YA MDOGO WAKE KANUMBA
Mazito mengine ambayo yamezidi kumpata Lulu ni maelezo ya mdogo wake Kanumba aitwaye Seth Bosco endapo yatasimamiwa na polisi yataweza kumpa hali ngumu mtuhumiwa huyo ambaye mwaka huu ametimiza miaka 18 kwa mujibu wa kinywa chake.

Habari zinasema kuwa, Bosco alieleza kwa polisi kile  alichokisikia wakati wa ugomvi wa Lulu na Kanumba ulipokuwa ukiendelea chumbani.

“Mdogo wake Kanumba naye (Bosco) yeye amekuwa akihojiwa mara kwa mara, mara ya kwanza alihojiwa  baada ya kifo cha kaka yake lakini  hata siku ya mazishi kule Kinondoni, alidakwa tena.

“Lakini katika maelezo yake amekuwa akiwaambia polisi maneno aliyoyasikia yakizungumzwa na Kanumba, kwa kweli da! Yanaweza kumuweka Lulu  katika wakati mgumu pia,” kilisema chanzo chetu.

HALI YA MITAANI
Hali inaashiria kuwa endapo Lulu angekuwepo siku ya mazishi ya Kanumba hata kwa kuonekana kwa dakika tano tu, mambo mawili yangeweza kumkuta, kama si kuumziwa basi zaidi ya hapo.

Wakati msafara ukielekea makaburini Kinondoni kutokea Viwanja vya Leaders Club, binti mmoja aliyefanana kwa mwonekano na Lulu akiwa amejifunika ushungi kichwani, alijiwa juu na baadhi ya waombolezaji, hasa vijana wakitaka kumfanyia kitu mbaya kwa madai ya kuhusika na kifo cha Kanumba.

Waombolezaji hao walisikika wakiimba pembeni ya binti huyo kuwa, walidhani shemeji kumbe sivyo hali inayompa picha Lulu kuwa, mtaani nako hakujakaa sawasawa dhidi yake.

Waombolezaji hao walizidi kumfuata mrembo huyo ambaye alikuwa ndani ya gari dogo, lakini kwa bahati nzuri, dereva wa gari hilo aliliondoa kwa kasi.

Hata hivyo, watu wanaomfahamu Lulu waliwaambia waombolezaji hao wenye hasira kuwa, waliyeamini ni Lulu hakuwa yeye.

AFANDE WA POLISI ALIMAANISHA NINI?
Wakati hayo yakiendelea, afande mmoja wa polisi ambaye hakufahamika kutoka kituo gani  akiwa amevaa sare za Kikosi cha Kuzuia Fujo aliwatawanya watu kwenye makaburi ya Kinondoni huku akisema, ‘sasa muondoke, hapa tumemaliza, tutakutana mahakamani.’

Kauli hiyo ilichukuliwa na baadhi ya waombolezaji kama ishara ya kuhakikishiwa kuwa, Lulu atafikishwa mahakamani wakati sehemu ya jamii inaamini kinyume.

Hata hivyo, juzi serikali ilisema hatima ya msanii huyo kwamba ana kesi ya kujibu au la iko mezani kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania (DPP).

LULU AKIMBIZWA HOSPITALI
Siku mbili kabla ya mazishi ya Kanumba, Lulu alikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam baada ya madai kuwa alizidiwa na maumivu yaliyotokana na ugomvi kati yake na marehemu.

Afande mmoja wa Kituo cha Polisi cha Oysterbay ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa sababu yeye si msemaji wa jeshi hilo, alikiri Lulu kupelekwa Mwananyamala kwa matibabu lakini akasema baadaye alirudishwa mahabusu.