Mabinti, wake za watu wamponza Mchungaji

MCHUNGAJI wa Kanisa la Baptisti la Makole katika Manispaa ya Dodoma, John Mwangafike ambaye pia ni Katibu wa Kanisa hilo Tanzania, amefukuzwa katika kazi hiyo ya kumtumikia Mungu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kukiuka kwake kwa makusudi maadili ya kichungaji.

Kwa mujibu wa barua ya kumfukuza mchungaji huyo ambayo gazeti hili ina nakala yake,

hatua hiyo imetokana na kikao cha uongozi wa Kanisa hilo kilichoketi Aprili, mwaka huu.


Barua hiyo ilieleza kuwa, Kanisa la Baptisti Makole limeamua kwa kauli moja kumfukuza

kwenye huduma mchungaji huyo kutokana na kukiuka kwa makusudi maadili ya kichungaji,
mojawapo ikiwa ni kuzini na kuzaa na waumini wake.

“Aidha Kanisa katika kikao cha Jumuiya ndogo ya Dodoma ya Aprili 15, mwaka huu, iliridhia wewe kufukuzwa katika huduma ya kichungaji hapa Kanisa la Kibatisti Makole,” ilisema sehemu ya barua hiyo.


Barua hiyo ambayo ilitiwa saini na Katibu wa Kanisa hilo, Daniel Njonde na Mzee Kiongozi wa Kanisa hilo Simon Marivey Pia ilimtaka Mchungaji huyo kukabidhi mali zote za Kanisa.


Mali hizo zilitajwa kuwa ni pamoja na hatimiliki ya eneo lote la Kanisa na ramani, nyumba aliyokuwa akiishi na familia yake, vifaa vya ofisi, mikataba ya CIT na Kanisa pamoja na ya watendakazi, mafaili ya watendakazi, mali ya huduma za mtoto, nyaraka zote za kanisa na huduma ya mtoto, vitabu, majarida, funguo zote za kanisa, huduma ya mtoto na posta.


Kwa mujibu wa barua hiyo mchungaji huyo alitakiwa kukabidhi mali hizo kwa niaba ya Kanisa jana saa nne asubuhi kanisani hapo ikiwa ni pamoja na kuondoka katika eneo hilo akiwa na familia yake. Katika barua hiyo mchungaji huyo aliambiwa kuwa, ubadhirifu wowote

utakaobainika kufanywa naye katika huduma ya mtoto kwa kipindi chote cha uongozi wake Kanisa litamchukulia hatua kali za kisheria.

Nakala ya barua hiyo pia ilitolewa kwa Kanisa hilo Makole, Mwenyekiti wa Stesheni ya Dodoma, Mwenyekiti Stesheni ya Mashariki, Mwenyekiti wa Stesheni ya Chilonwa, Mwenyekiti Jumuia ndogo Dodoma, Mwenyekiti Kanda ya Pwani na Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu.


Mwandishi wa habari hizi alifika jana kanisani hapo, lakini hata hivyo mchungaji huyo hakuwepo na hata namba yake ya simu ilikuwa haipatikani.


“Mchungaji hapa hayupo, hata nyumbani kwake haonekani kuna familia yake tu tumejaribu kumtafuta kwenye simu lakini hapatikani kwa hiyo sifahamu lolote japo ilikuwa leo alitakiwa kukabidhi mali za Kanisa na pia kutoka kwenye nyumba ya kanisa,” alisema mmoja wa watu wanaofanya kazi kanisani hapo ambaye hakutaka kutaja jina lake.


Alisema kuwa hafahamu kitu gani kitafuata, lakini anajua kutakuwa na kikao cha kujadili suala hilo kwani mchungaji huyo alitakiwa kuachia nyumba ya Kanisa kama alivyoelekezwa kwenye barua.


Awali, habari kutoka ndani ya Kanisa hilo zinasema kuwa, Askofu na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kanisa la Baptisti mkoani hapa, Emmanuel Mwakandulu alisaini barua ya waumini na wazee wa Kanisa hilo, waliotaka Mchungaji huyo asimamishwe kwa tuhuma za kuzaa na waumini, akiwemo msichana wake wa kazi na mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mtu ambaye licha ya kuwa na mtoto moja naye, sasa ni mjamzito.


Kusimamishwa kwa mchungaji huyo kuliridhiwa na washirika 47 na wazee wa Kanisa hilo.

Kulingana na tuhuma za mchungaji huyo, waumini na viongozi walitaka mchungaji huyo aondolewe kwenye huduma baada ya kukaidi kujiuzulu alipotakiwa kufanya hivyo.

Hatua ya kumtimua kiongozi huyo imefanyika kulingana na Imani ya Kibaptisti na Katiba ya Kanisa hilo kifungu Na. 24(9), 27(C) na (F) (10) vinavyozungumzia ukosefu wa maadili.


Waumini wote wa Makole na wajumbe (Wachungaji) wanne waliridhia Mchungaji Mwangafike aachishwe huduma ya Kichungaji.


Kwa mujibu wa muhtasari wa kikao cha Wachungaji na Viongozi wa Jumuiya Ndogo ya Dodoma cha Machi 9, mwaka huu ajenda namba Sita (6) iliyohusu tuhuma zinazomkabili Mchungaji John Paulo Mwangafike ilisomwa bila kujadiliwa, ambapo ilikubalika kwa wajumbe wote, ajenda hiyo isijadiliwe kwa kuwa mtuhumiwa (Mchungaji Mwangafike)

hakuwapo.

Hata hivyo waliteuliwa wajumbe (wachungaji) watano wakamuone na kumjulisha yanayojiri.

Ajenda nyingine ilikuwa ni juu ya tuhuma za mchungaji huyo kumnyang’anya Denis Chiyombo mke ambaye ni muumini wa kanisa hilo na kuzaa naye mtoto mmoja na pia kumpa ujauzito alionao sasa.

Aidha, anatajwa kuzaa watoto watatu na mfanyakazi wa ndani ambaye hata hivyo jina lake linahifadhiwa na kuzaa mtoto mmoja mmoja na waumini wake wawili (majina tunayo).


Inaelezwa katika kikao hicho na wajumbe waliofika kwake, alikanusha kuwa na watoto nje ya ndoa, akisema wanaomwita baba ni `watoto wa kiroho’.


Aidha, inaelezwa Mchungaji huyo alikiri kusafirisha kwa jina la Kanisa chakula kwenda Malawi, akisema waumini wa Kanisa hilo nchini humo wako katika njaa, ingawa hakikuwafikia.


Juhudi za gazeti hili kumpata mchungaji huyo kuzungumzia tuhuma hizo hazikuzaa matunda, kwani mara zote alipofuatwa nyumbani kwake hakupatikana na pia hakupatikana kwa simu yake ya mkononi.

chanzo HabariLeo