MBOWE ADAI KUWA ATAJIUZURU SIASA ENDAPO CCM ITASALIMIKA 2015

Mwenyekiti wa wa Chadema, Freeman Mbowe
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.


Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.

“Wajibu wa Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu (kipindi cha Mwinyi). Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu  (Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema hatuwezi kukubali na moto huu tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM itasalimika nitajiuzulu siasa.”

“CCM ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na wafanyakazi wa kipato cha chini, ilijenga mshikamano baina ya Watanzania wote bila kujali ukabila. Tanzania ina makabila zaidi ya 120, lakini tunaishi kama mtu na ndugu yake, leo taifa limegawanyika vipande huku maadili ya uongozi yakiporomoka,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza kusikitishwa kwake na umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya kuwapo rasilimali nyingi zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho. Alisema kumekuwa na ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na licha ya wananchi kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa hiyo ya kusini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma muhimu za kijamii kama zahanati na shule.