Dk. Slaa (kulia) akiwa jukwaani na mchumba wake Josephine Mushumbuzi |
Dk. Slaa akiwa na Rose Kamili |
Ile
ndoa kati ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa na mchumba
wake Josephine Mushumbuzi iliyopangwa kufanyika Jumamosi ijayo (Julai
21) sasa iko njia panda baada ya Jaji Lawrance Kaduli wa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam anayesikiliza pingamizi la ndoa hiyo lililowekwa
na aliyekuwa mke wa Dk. Slaa, Rose Kamili kuamuru kuwa suala hilo
lifikishwe tena kortini Agosti 14, ikiwa ni baada ya kupita kwa tarehe
iliyopangwa kwa ajili ya kufungwa kwa ndoa hiyo.
Mahakama
hiyo imepanga kuwa Agosti 14 mwaka huu isikilize kesi hiyo ya
kusimamisha ndoa ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa na
mchumba wake Josephine Mushumbuzi inayotarajiwa kufungwa katika wilaya
ya Karatu mkoani Manyara.
Jaji
Kaduli, leo ameitaja kesi hiyo namba 4 ya mwaka 2012, iliyofunguliwa
na mke wa Dk, Slaa, Rose Kamili ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum
(Chadema). Jaji huyo aliwataka Dk Slaa na Josephine wajibu pingamizi
hilo la ndoa yao kwa njia ya maandishi kabla ya Julai 30, mwaka huu.
Pia
alimtaka Rose Kamili kupitia wakili wake, Joseph Thadayo kama
watakuwa na majibu yoyote wayafaili Agosti 7, mwaka huu na kwamba
baada ya taratibu hizo kufanyika, Agosti 14 mwaka huu ataisikiliza kesi
hiyo.
Kwa
maana hiyo, ndoa hiyo iliyotajiwa kufungwa Jumamosi ijayo ya Julai
21, haitafungwa hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa maamuzi juu ya
maombi hayo.
Katika
kesi hiyo dhidi ya Dk Slaa na mchumba wake Josephine Mushumbusi,
mlalamikaji Rose Kamili anaiomba Mahakama kusimamisha ndoa hiyo
iliyopangwa kufungwa wilayani Karatu mkoa wa Manyara.
Rose
pia anaiomba mahakama imuamuru Dk. Slaa kumlipa Sh. milioni 50 kama
fidia aliyotumia kujihudumia pasipo matunzo ya mumewe huyo.
Mbunge
huyo kupitia wakili wake Thadayo, anaiomba pia mahakama iamuru
Mushumbuzi amlipe Sh. milioni 500 kama fidia ya maumivu aliyoyapata
kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika
hati hiyo ya madai, mbunge huyo anadai kuwa ndoa inayotarajiwa
kufungwa kati ya Dk.Slaa na Mushumbuzi ni batili kwa sababu kuna ndoa
nyingine halali na inayoendelea kuishi kati ya Dk. Slaa na yeye (Rose
Kamili) iliyofungwa mwaka 1985.
Alidai
baada ya kufugwa kwa ndoa hiyo, Juni 18 mwaka 1987 walifanikiwa
kupata mtoto wa kike anayeitwa Emiliana na baadaye Septemba 23 mwaka
1988, walipata mtoto mwingine wa kiume aitwaye Linus Amsi.
Katika
uhusiano wao, Dk. Slaa akiwa ni Padri wa Kanisa la Roman Katoliki,
alifanya taratibu zilizomwondosha katika nafasi hiyo ya upadre na
kuanza maisha ya familia.
Baada
ya taratibu hizo, jamii ya Watanzania iliwatambua kama mume na mke
ambapo hata kumbukumbu za hati za kimataifa kama za kusafiria
ziliwatambua wao kuwa ni wanandoa.
Rose
Kamili aliendelea kudai katika maelezo hayo kuwa yeye na Dk. Slaa
waliishi maisha ya ndoa yenye amani, yaliyowawezesha kupata mali kadhaa
walizomiliki kwa pamoja ikiwemo nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba
609 kitalu E, nyumba ya makazi iliyopo kijiji cha Gongali huko Karatu na
vifaa mbalimbali vya nyumbani.
Hati
ya mashtaka imeendelea kueleza kuwa, uhusiano kati ya Slaa na mkewe
Kamili, ulianza kuharibika mwaka 2009, baada ya Slaa kuwa na
mahusiano na mwanamke mwingine kinyume cha sheria. "Tangu mwaka huo
2009, Slaa akaitelekeza familia yake kwa kutoipatia huduma," imeeleza
hati hiyo.
Kamili
anaiomba mahakama iamuru kuwa yeye na Slaa bado ni mke na mume na
kwamba Mushumbusi aliingilia ndoa yao hivyo mahakama izuie ndoa
inayotajiwa kufungwa Julai 21, mwaka huu huko Karatu mkoani Manyara.
Kamili pia amewasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo.
Kamili
akamweleza askofu mkuu huyo wa jimbo Katoliki la Dar es Salaam, kuwa
moja ya Parokia za Dar es Salaam zina taarifa ya ndoa hiyo.