Na: Maggid Mjengwa,
WATANZANIA
tumekumbwa tena na balaa la ajali kubwa ya meli kuzama. Ni wakati sasa
wa kujifunza kutokana na yaliyotokea huko nyuma.
Maana
ajali ya Mv Skagit inaonekana dhahiri kuchangiwa na uzembe. Na uzembe
kwa nchi yetu unalelewa na mfumo mbovu. Na mfumo mbovu unatokana na
Katiba mbovu.
Maana,
ni katika mazingira haya ya kufanya mambo ya hovyohovyo ndipo
tunapokuwa na wanasiasa wa hovyohovyo wenye kuhusika pia na biashara
ya uchukuzi na usafirishaji wa abiria.
Ni
vigumu kwa mfumo wetu wa sasa, kwa watendaji wa vyombo au taasisi
zisizo huru kikatiba na kisheria kuweza kuwasimamia wafanyabiashara
dhalimu ambao miongoni mwao wamo baadhi ya wanasiasa wetu.
Tuna
lazima sasa kupitia Katiba yetu ijayo, kuvipa nguvu za kisheria vyombo
na taasisi zetu muhimu kwa nchi yetu. Tuwe na vyombo na taasisi huru
ambazo utendaji wake hauwezi kuingiliwa kirahisi na mamlaka nyingine.
Fikiri
leo kama tungekuwa na utaratibu wa kwamba mmiliki wa chombo cha majini
au angani na atakayebainika kuingiza nchini chombo kilicho chini ya
viwango vinavyokubalika kimataifa na hata chombo hicho kikasababisha
ajali ya kuua raia kuwa mmiliki huyo atafungwa jela na kufilisiwa mali
zake? Naamini, tungekuwa na vyombo madhubuti na ajali zingetokea kwa
bahati mbaya kwa maana yake halisi.
Ni nini basi cha kujifunza kutoka kwenye ajali iliyopita ya Mv Spice Islanders?
Ikumbukwe,
Ripoti ya Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa Meli ya Mv Spice
Islanders ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Mustafa
Aboud Jumbe pamoja na wahusika wengine wachukuliwe hatua za kisheria na
kinidhamu kutokana na uzembe waliofanya na kusababisha kuzama kwa Meli
hiyo. Mpaka leo hii hatujasikia adhabu walizopewa wahusika wa ajali ile.
Maana,
bado tunakumbuka kuwa, ripoti ile ilibainisha kuwa miongoni mwa watu
ambao walibainika na makosa katika ajali ya Mv Spice Islanders ni pamoja
na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Haji Vuai
Ussi, Mkuu wa kituo cha usimamizi wa usalama wa vyombo vya baharini wa
Shirika la Bandari, Usawa Khamis Said na Kaimu Mdhibiti wa Bandari ya
Malindi, Sarboko Makarani Sarboko.
Wengine
ni pamoja na Wanahisa wa Kampuni inayomiliki meli hiyo Jaku Hashim Ayub
ambaye ni Mwakilishi na Mbuge wa Jimbo la Muyuni, Salim Said Mohammed,
Makame Hasnuu Makame na Yussuf Suleiman Issa.
Alikuwamo
pia nahodha wa meli Said Abdallah Kinyanyite na wasaidizi wake, Ofisa
usafirishaji wa Shirika la Bandari Hassan Mussa Mwinyi na Mkaguzi wa
Meli wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini, Juma Seif Juma.
Ndiyo, wakati bado hatuna hakika ya hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya wahusika hawa leo tunaomboleza msiba mwingine kwa taifa.
Hakika,
inasikitisha sana, kuwa hata mwaka haujatimu kukumbuka ajali iliyopita
ya Septemba 9, 2011, Watanzania tunapatwa na msiba mwingine. Na misiba
yote miwili inatokana na uzembe na wala si ya kusingizia ‘Kazi ya
Mungu’.
Watanzania
sasa tunataka kuona hatua kali za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa,
tena kwa haraka dhidi ya wahusika waliochangia kwenye ajali ile ya Mv
Skagit.
Kwa
kuanzia jina la mmiliki wa meli liwekwe hadharani. Na Tume
itakayochunguza ajali hii itabaini kuwa mwenye meli ameingiza chombo
chakavu, basi, awe wa kwanza kutolewa mfano.
Maana,
kama taifa, bila kuwa wakali katika haya ya msingi, basi, tunahatarisha
usalama wa taifa letu pia. Kamwe tusiruhusu hilo kutokea. Nahitimisha.