Watoto wafanyiwa unyama Segerea

WATOTO wenye umri chini ya miaka 18 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali au waliohukumiwa huwekwa sehemu moja na watu wazima katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam na baadhi yao kuingiliwa kinyume na maumbile na kuharibiwa vibaya.
Tuhuma hizo nzito dhidi ya magereza zilibainika wakati Kamati ndogo ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, ilipokuwa ikiwasilisha kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inayoongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kile ilichokiona katika gereza hilo baada ya kufanya ziara.


Kamati hiyo ilitoa taarifa yake katika kikao kilichofanyika Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam wiki iliyopita ambacho pia kilihudhuriwa na maofisa mbalimbali wa Jeshi la Magereza akiwemo Kamishna wake Mkuu, Augustino Nanyaro.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kuwa Kamati hiyo ya Ukimwi ilieleza kwamba watoto chini ya miaka 18 wanaofika katika gereza hilo kwa makosa mbalimbali, utambulisho wao huonyesha kuwa wana miaka 19 hadi 20.

Taarifa hizo zilidai kwamba watoto hao ambao hukaa na wakubwa mchana, usiku huhamishiwa sehemu nyingine na kuingiliwa kinyume na maumbile kutokana na mazingira yalivyo ya kukosa pa kukimbilia.