Madaktari Bingwa Wamjibu JK

 AGIZO la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na mgomo kuacha kazi limechukua sura mpya baada ya madaktari bingwa ambao awali hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi huyo wa nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini.
Badala yake, madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao juzi, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka, walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapowarejesha kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa.
Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura jana na kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi wa mabingwa hao Dk. Catherine Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao.
“Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu… kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi.
“Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo.
Soma zaidi:http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=37661