MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI TANZANIA ALAANI KITENDO CHA SERIKALI KULIFUNGA GAZETI LA MWANAHALISI


MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda
SERIKALI imelifungia Gazeti la Mwanahalisi kwa kile ilichodai kuwa mwenendo wake wa kuandika habari na makala ni wa kichochezi, uhasama na uzushi.Hii ni mara ya pili kwa Serikali kulifungia gazeti hilo. Hata hivyo, safari hii imelifungia kwa muda usiojulikana kuanzia Julai 30, mwaka huu. Mara ya kwanza lilifungiwa mwaka juzi kwa kipindi cha miezi mitatu likidaiwa kumchonganisha Rais na familia yake.
Akitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam kwa niaba ya Msajili wa Magazeti, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari – Maelezo, Fabian Rugaimukamu alisema jana kwamba makala hizo zimesababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Alisema hivi karibuni gazeti hilo katika toleo lake namba 302, la Julai 11 hadi 18, mwaka huu na toleo la Julai 25 hadi Agosti Mosi, lilichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.

“Tumeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana Gazeti la MwanaHalisi. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Kifungu namba (25) (1), adhabu hiyo itaanza Julai 30 (jana), 2012 kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba 258 lililochapishwa Julai 27,” alisema Rugaimukamu.
Alisema Mhariri wa gazeti hilo ameitwa na kuonywa mara nyingi lakini, hakutaka kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Alisema mara zote katika utetezi wake amekuwa akinukuu Kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi ambacho kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kusema kwa makusudi amekuwa akiacha kukinukuu Kifungu cha 30 cha Katiba, kinachoweka ukomo wa uhuru wa habari.

Kufutia matukio hayo, alisema Serikali inawataka wamiliki, wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.

Alisema kama ilivyoelezwa bungeni wakati wakuwasilisha bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni, waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya taifa na uzalendo.

Alisema kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa makusudi vitatoa taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini.

MwanaHalisi wasikitika
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, Mhariri wa Mwanahalisi, Jabir Idrissa alisema umemsikitisha kwani umechukuliwa kwa kutumia sheria ambayo ni moja kati ya zile ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwamba ni kandamizi.

Idrissa alisema hadi jana mchana kampuni yao haikuwa imepata taarifa rasmi za uamuzi huo wa Serikali lakini, aliupinga akisema unalenga kudhoofisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Kama unavyojua, Waziri ametumia sheria ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwamba ni kandamizi, hii (Sheria ya Magazeti) ni moja ya sheria 43 ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwamba ni kandamizi tangu miaka ya 1990. Kwa hiyo, siwezi kusema tutachukua hatua gani kwani tunahitaji kukaa na kujadili kwanza uamuzi huo,” alisema.

Jukwaa la Wahariri
Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alisema hatua hiyo ya Serikali ni kitisho dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Alisema wakati dunia inaendelea kufungua milango ya uhuru wa vyombo vya habari, demokrasi na uhuru wa uhariri, inashangaza kuona nchini hali ni tofauti na Serikali inataka kurudisha mambo nyuma.

Alisema malalamiko juu ya sheria kandamizi dhidi ya vyombo vya habari yalitolewa mbele ya Rais Jakaya Kikwete katika sherehe ya kutoa Tuzo kwa Waandishi bora wa habari, lakini inasikitisha kuona ukandamizaji, vitisho na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari unazidi kushika kasi.

Kibanda alisema hadhani kama uamuzi huo wa Serikali unatokana na MwanaHalisi kufanya kazi zake bila kuzingatia weledi wa kitaaluma, bali pengine ni kutokana na msukumo wa hofu ya mambo yanayoandikwa na gazeti hilo kwamba yanaiweka pabaya Serikali.