SHEHATA AMKINGIA KIFUA BRADLEY.

Hassan Shehata.
KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Misri, Hassan Shehata amesema pamoja na kusikitishwa kwa kusindwa kufuzu kwa kikosi hicho katika michuao ya Mataifa ya Afrika mwakani lakini suala hilo lilitegemewa kutokea. Shehata amesema kuwa kinachotakiwa sasa hivi timu hiyo ni kujipanga na kuangalia changamoto zinazowakabili huko mbele ili kuhakikisha wanarudisha heshima yao kama mabingwa soka Afrika. Kocha huyo aliendelea kusema kuwa Misri imeshinda mataji matatu ya Afrika mfululizo hivyo ni kawaida kushika kiwango lakini anaomba wazinduke mapema ili kurejea makali yao kama zamani. Shehata pia alimkingia kifua kocha wa timu hiyo Bob Bradley na kusema kuwa amesaidia kujenga kikosi kizuri na wanatakiwa waendelee kumpa ushirikiano kwani anafanya vizuri katika michezo ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo anaamini ataweza kukipeleka kikosi hicho nchini Brazil mwaka 2014. Hata hivyo taarifa kutoka kwa msemaji wa Chama cha Soka cha nchi hiyo-EFA, Azmey Megahed amesema kuwa kutakuwa na kikao cha bodi ili kujadili mustakabali wa Bradley.