Uchambuzi Na Utabiri Wa Olle; Italy Vs Spain, Nani Atashinda Leo?

 
Wapenzi wa soka,
Naandika nikiwa Barcelona. Leo Italy na Spain wanacheza fainali za EURO. Naamini, mechi hii ni ngumu sana kutabirika. Kwanini?
Italy na Spain walishakutana kwenye mechi za makundi kwenye Euro hii. Na matokeo yakawa 1-1. Ilikuwa mechi ngumu na timu zilikuwa na nguvu sawa. Kama ningetabiri matokeo ya leo, basi, ningesema itakuwa droo. Lakini, leo ni fainali na timu moja lazima ibebe kombe.
Ikumbukwe, Spain imeingia fainali bila kuwa na wafungaji wa kuaminika ambao wamepachika mabao 8. Tukumbuke pia kati ya mabao hayo 8, manne yalipatikana katika mechi moja dhidi ya Irland. Na imekuwa na wafungaji watano tofauti. Hakuna hata mchezaji mmoja wa Spain aliyefunga mabao zaidi ya mawili katika mashindano haya. Hivyo, Spain haina mshambuliaji wanayemuamini zaidi katika kufunga mabao.

Katika fainali zilizopita za Kombe la Dunia Spain waliwekeza zaidi kwa David Villa ambaye alifunga mabao matano katika fainali zile.
Mwaka huu, tunaweza kabisa kusema, kuwa kinachokosekana zaidi kwa Spain ni mshambuliaji wa kuaminika katika kufunga mabao. Spain imemchezesha mbele Cesc Fabregas katika mechi za Euro lakini amefunga mabao mawili tu.
Kwa ukweli kabisa, Fabregas ni kiungo na si mshambuliaji. Na nadhani cha akili kabisa anachoweza kukifanya kocha Del Bosque usiku huu ni kumpanga mshambuliaji kama Torres au Negredo.
Italy wamefanya vema hadi sasa. Wamekuwa na mechi ngumu kwa mfano walipokutana na Kroatia, na mechi ile walitoka sare. Mfano mwingine walipocheza na Uingereza , walishinda kwa penalti.



Nilikuwepo uwanjani kuona mechi ya Italy dhidi ya Ujerumani. Ukweli sijawahi kuwaona Italy wakicheza soka safi na kumiliki mpira kwa muda mrefu wa mchezo.
Nilichokipenda kwa Waitalia ni kuwa mara tu walipokamata mpira walipeleka mbele mashambulizi. Na katika mechi yao ya leo dhidi ya Spain, Italy wana ‘ bunduki’ kali kabisa wanayoitegemea. Si nyingine, bali ni Mario Balotelli ( Super Mario)


Na huyu, kwa mtazamo wangu, ndiye anayeweza kuamua hatma ya mechi ya leo. Ikumbukwe pia, Italy ndio timu pekee iliyopachika bao nyuma ya nyavu za Spain katika Euro hii-
Na utabiri wangu wa leo ni huu; Italy itashinda na kutwaa Kombe kwa penalti. Na tusubiri tuone!
Olle, Barcelona.