WANAOONDOKA TIP TOP NINI KINAWAKUTA?

 
NI jambo la kawaida mtu kusaka ulekeo mwingine wa maisha endapo atangundua kuwa sehemu aliyokuwa awali haimfikishi kwenye ndoto za kufanikiwa kimaisha zilizojaa kwenye halimashauri ya kichwa chake.

Kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya hasa wanaonza safari ya kusaka mafanikio kimuziki wakiwa ndani ya makundi imekuwa ni kawaida kujiweka pembeni na kuamua kutoka ‘solo’ ili kutafuta mafanikio zaidi kila wanapobaini kuwa ndani ya kundi walilopo bado kuna kiza.

Miaka michache iliyopita ndani ya gemu ya muziki wa kizazi kipya nchini unaobeba jina la Bongo Fleva tumeshuhudia kuibuka kwa makundi kadhaa ya muziki huo yalioundwa na vijana kwa lengo la kuweka nguvu ya pamoja na hatimaye kutusua (kufanikiwa) kimuziki.

Katika hili wapo ambao wamefanikiwa na wengine waliingia kwa nguvu lakini wakafa kibudu (bila mafanikio) na pia kuna waliofanikiwa lakini wakiwa tayari wamesambaratika vipande vipande.
Kwa wakati huu hakuna asiyefahamu uwepo wa kundi la Tip Top Connection lenye maskani yake pande za Manzese likiwa chini ya Hamad Ally ‘Madee’ ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikiwa kubaki kwenye ‘levo’ za juu ingawa tayari limeshaondokewa na nyota wake kadhaa ambao walikuwa wanaring’arisha ipasavyo.
Hakika kwenye mafanikio ya Tip top huwezi kuacha kuyataja majina kama Keisha, Kassim Mganga, Desso, MB Dogg, Spark, Z anto na sasa Dogo janja ambao licha ya kuwa hawakuwa na nafasi kubwa ‘kivile’ lakini mchango wao ulikuwa mkubwa ndani ya kundi.
Hakika wanamuziki hawa wakiwa ndani ya kundi hilo walipata mafanikio makubwa kupitia vibao vyao kadhaa vilivyowafanya kuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa Bongo fleva, lakini ajabu ni kuwa nyota zao zimezima ghafla na kuwaacha kizani waliokuwa mashabiki wa kazi zao.
Kwa Kassim unaweza kusema bado yupo kwenye gemu ingawa tangu kujiweka pembeni na Tip Top mwendo wake umekuwa wa kujikongoja kiasi kwamba imenza kuleta hofu kuwa huenda ndani ya siku chache zijao nae atapotea kama walivyoptea wengine.
Keisha, Desso, MB Dogg, Spark, Z anto ni kam hawapo kabisa kwenye ulimwengu wa muziki wa kizazi kipya kwani nyimbo zao hivi sasa haziko tena kwenye masikio ya watu na hata wanapotoa nyimbo mpya basi zinaishia kusikika vichochoni na mwisho wa siku zinapotea.
Maswali ni mengi lakini lililokubwa ni kuwa ni jambo gani linawakuta nyota hao mpaka wanashindwa kuonyesha uwezo wao kimuziki wakiwa nje ya Tip Top,? Je ni kweli kuwa kuna mbinu chafu zinazofanywa nyuma yao ili kuwapoteza kimuziki kama ambavyo imekuwa ikidaiwa mitaani.

Ama uwezowao ulikuwa mdogo na kung’ara kwao kulichangiwa na kuwepo kwa wakali wengine ndani ya kundi walilokuwa wakilitumikia? Au wana ugomvi na baadhi ya vyombo vya habari? Na kama kun amtu anafanya juhudi za kuwabania yeye ana nufaika nini n akutokufanikiwa kwao nje ya kundi hilo? hakika majibu yako kizani.

Kinachoumiza kichwa zaidi hivi sasa ni kuhusu maajaliwa ya Dogo Janja ambaye ni juzi tu amejiondoa kutoka kundi hilo nini kinafuata kwenye kipaji chake cha muziki?

Tusubiri kuona nini kinatokea, ingawa ukweli unabaki kuwa kizani juu ya kinachowapata nyota wanaoondoka ndani ya Tip Top kwenda kuanza maisha mapya kimuziki.