ATCL yasitisha mkataba na kampuni ya Aero Vista

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la ATCL Kapteni Milton Lazaro akizungumza na waandishi wa habari juu ya kushitisha kwa mkataba baina ya shirika hilo na kampuni ya Aero Vista Dubai ambayo ilikodisha shirika hilo ndege aina ya Boeing  737-500.
SHIRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL) limesitisha mkataba wake na kampuni ya Dubai ya Aero Vista kutokana na kuwa makubaliano yaliyofikiwa mapema mwezi Mei hayakuleta maafanikio yaliyotarajiwa.

ATCL ilikodi ndege aina ya Boeing 737 – 500 yenye uwezo wa kubeba abiria 108 mnamo mwezi wa tano ambayo imekuwa ikiitumia kufanya  safari za Dar es Salaam – Kilimanjaro- Mwanza na baadae kuzitumia katika safari nyingine ya Dar es Salaam – Hahaya (Comoro) iliyozinduliwa mwezi uliopita.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Kapteni Milton Lazaro alisema kuwa shirika limefikia uamuzi huo baada ya kugundua kuwa shirika halipati faida iliyokusudiwa kabla ya kusaini mkataba huo.

Aidha, Lazaro alisema kuwa shirika lipo katika mazungumzo na kampuni nyingine ili kuafikiana katika kufanya biashara pamoja na kuongeza kwamba mazungumzo hayo yanatarajia kukamilika katika wiki chache zijazo.

 “Tumeamua kusitisha mkataba tuliosaini na kampuni ya Aero –Vista kutokana na ukweli kuwa mkataba huwo haujatuletea mafanikio tulieyeyekusudia. Kuna uwezekano wa kujadiliana upya na tunaweza tukaingia nao katika mkataba mpya baada ya mazungumzo kama wanaweza kuondoa baadhi ya vipengele ambavyo si vizuri kwetu kama kampuni.

 “Abiria ambao tayari wameshakata tiketi katika kampuni yetu hawana sababu ya kuwa na wasiwasi sababu tayari tumeshawakatia tiketi katika mashirika mengine ambayo na safari zao zitaendelea kama walivyopanga,” alisema Lazaro.

Aliongeza kuwa shirika hilo la ndege la taifa litarudisha safari zake Dar –es Salaam- Kilimanjaro-Mwanza baada ya kukamilika kwa matengenezo ya ndege ya shirika hilo aina ya Dash 8Q-300 ambayo ipo katika karakana ya shirika hilo kwa sasa.

Pia, Kapteni Lazaro alisema kuwa safari ya Dar es Salaam – Kilimanjaro – Mwanza ndiyo safari pekee itakayoathirika kutokana kusitishwa kwa mkataba huwo na kuongeza kuwa shirika litaendelea na safari zake za Dar es Salaam – Hahaya kama kawaida.

 “Tunaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza. Wateja wasifikirie kuwa hatupo kabisa kwenye biashara. Tutaendelea na safari zetu za Dar es Salaam – Hahaya (Comoros) kwa kipindi hiki. Ni safari za Dar es Salaam – Kilimanjaro – Mwanza pekee ndizo zitakazodhurika katika kusitishwa kwa mkataba huu,” alisema.