Chama
Cha Walimu Tanzania-CWT-kimetangaza kusitisha rasmi mgomo wa walimu
na hivyo kuwataka walimu wote nchini kurejea kazini mara moja kuanzia
leo ili kutekeleza majukumu yao ya kila siku kama kawaida.
Akitoa
tamko la CWT kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam ikiwa
ni siku moja baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kukiagiza Chama
hicho kitoe maelekezo kwa wanachama wake kurudi kazini, Rais wa Chama
hicho GRATIAN MUKOBA amesema walimu wanarudi kazini wakiwa wamekata
tamaa kutokana na hukumu hiyo.
Amefafanua
kuwa walimu wanaporudi kazini bila kuwa na mawazo yaliyotulia,
utendaji wao utaathirika hivyo Chama kinatoa wito kwa Serikali kukutana
na CWT kwa haraka ili kuendeleza majadiliano ya Madai mapya ya
Walimu.
Kuhusu
kulipa fidia ya hasara waliyoipata wanafunzi, Chama hicho kimesema
kinasubiri taarifa rasmi ya Serikali kuhusu hasara hiyo kwa kuwa hakina
uwezo wa kufahamu hasara waliyoipata wanafunzi.
Kwa mujibu wa Mwalimu MUKOBA wenye uwezo wa kuwasilisha hasara hiyo ni mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Serikali.
Hapo jana Chama hicho kilipongeza kauli ya Rais JAKAYA KIKWETE yakusema Serikali inajali na kuthamini mchango wa Walimu nchini.