MWAKILISHI
wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Lisa Jensen ameanza
kufanya kweli katika michuano hiyo baada ya kufanikiwa kuingia kumi bora
ya shindano la Top Model, hivyo kumuongezea pointi zaidi kabla ya
fainali za kinyang’anyiro hicho.
Habari
zilizopatikana kutopka Mongolia ambako shindano la Miss World
litafanyika, zimepasha kuwa Lisa alikuwa mwiba mchungu kwa washiriki
wengine kutokana na uwezo wake mkubwa, huku akionesha kipaji cha aina
yake katika shindano hilo lililofanyika juzi usiku nchini
humo. Akithibitisha habari hizi, Afisa Habari wa Kamati ya Miss
Tanzania, Haidan Ricco alisema Lisa ni mmoja kati ya wawakilishi watatu
kutoka Bara la Afrika ambao wamefanikiwa kupenya na kuingia katika
nafasi hiyo muhimu.
Waafrika
wengine waliofanikiwa kupenya katika kumi bora ya shindano hilo kabla
ya siku ya fainali ya Miss World ni mrembo wa Afrika Kusini na
Shelisheli. Lisa amefanikiwa kufanya kweli na kuwatoa kimasomaso
Watanzania ambao kwa sasa wanajikuta katika hali mbaya kutokana na
wanamichezo wake waliopo katika Michuano ya Olimpiki wakifanya vibaya.
Kutokana
na kuingia kumi bora, Lisa bado ana kazi kubwa ya kuhakikisha
anapambana ndani ya wiki hii wakati mshindi wa Top Model atakaposakwa
rasmi. “Kwetu sisi ni faraja kubwa mno, kwani tunaamini Lisa
ataiwakilisha vema Tanzania na huu ni mwanzo mzuri kwake,” alisema
Ricco, huku akitaka Watanzania wamuombee kabla ya kufanyika shindano la
Miss World hapo Agosti 18, ili aweze kufanya kweli.
Shindano la Miss Tanzania kwa sasa linadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s, ambacho kinazalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania.