Hatma ya mgomo ni leo mahakamani


HATIMA ya mgomo wa walimu unaoendelea nchini kote sasa itajulikana leo, ambapo  Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi itakapotoa uamuzi ambao ama utaridhia au utazuia mgomo huo.Mgogoro baina ya Serikali na walimu ulishindwa kupata usuluhishi na hapo Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Katibu Mkuu Utumishi, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ilifungua mgogoro wa kikazi mahakamani hapo.
Sambamba na mgogoro huo, pia Serikali iliomba mahakama itoe zuio la muda la mgomo huo ili kusubiri uamuzi wa mahakama katika mgogoro huo wa kikazi.

Juzi, Mahakama Kuu chini ya Jaji Sophia Wambura baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu maombi ya kutoa zuio hilo la muda la mgomo ilipanga kutoa uamuzi kesho.

Wakati wa usikilizwaji wa hoza za pande zote, Mawakili wa Serikali Wakuu (PSAs) Obadia Kameya na Pius Mboya walidai kuwa mgomo huo si halali kwa kuwa haukutimiza masharti ya mgomo.

Alisema kwa kuwa walimu ni kundi la watumishi wa umma,
wanapotaka kugoma wanapaswa kutumia Sheria ya Majadaliano namba 19 ya 2003.

Alisema kifungu cha 26 cha sheria hiyo kinatoa masharti matatu,
kuwapo kwa mgogoro au madai, kuendesha kura ya kuunga mkono au kutokuunga mkono kuwapo kwa mgomo ambayo itasimamiwa na afisa wa umma na kwamba kuwepo kwa mgomo kutamuriwa kwa uwingi wa kura za wanachama.

Kameya alisema walimu hawakutimiza masharti hayo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa ya saa 48 badala ya siku 60 kama sheria inavyowataka.

Kwa upande wake wakili wa CWT, Gabriel Mnyele akijibu hoja hizo alidai kuwa walimu hao wametimiza masharti ya mgomo na kuiomba mahakama isikubali kutoa zuio ili kuilazimisha serikali kutekeleza madai yao.

Alisema kama mahakama itatoa zuio hilo serikali wajibu maombi hao wataumia kwani serikali itasahau madai yao.

Alisisitiza kuwa kuwa ikiwa haitatoa zuio hilo itaisukuma serikali kutekeleza madai yao na kuitaka serikali iache kukimbilia mahakamani ili kuomba zuio la migomo bali itekeleza madai ya wajibu maombi hao