UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umepuliza kipenga cha uchaguzi wa viongozi wa chama hicho, ngazi ya taifa. Katika uchaguzi huo nafasi mbalimbali zitagombewa ikiwa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa umoja huo taifa, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa nafasi sita kwa Tanzania Bara na nafasi nne kwa visiwani. Nafasi nyingine ni Wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, nafasi tano kwa Tanzania Bara na nafasi tano kwa visiwani pamoja na mjumbe mmoja wa kuwakilisha UVCCM katika vikao vya Jumuiya ya Wanawake (UWT) na Wazazi.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela ilisema kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Agosti 28 hadi Agosti 30 mwaka huu. Alisema kazi ya kuchukua fomu kwa wanachama wenye sifa itaanza Agosti Mosi, mwaka 2012 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi Agosti 6, saa 10:00 jioni.Shigela alisema kuwa mwombaji wa nafasi zilizotajwa anaruhusiwa kuchuka na kurejesha fomu katika Ofisi za UVCCM mkoa, Ofisi Kuu ya Zanzibar na makao makuu ya Jumuiya hiyo taifa wakati nafasi ya Mwenyekiti wa UVCCM Taifa na Makamu Mwenyekiti watatakiwa kurejesha fomu hizo kwa Katibu Mkuu wa UVCCM taifa Makao Makuu Dar es Salaam.
Alisisitiza kuwa mwombaji wa nafasi hizo za uongozi anatakiwa awe mwanachama hai wa UVCCM na CCM na anayetimiza haki, wajibu na masharti ya uanachama ikiwa ni pamoja na kuwa Raia wa Tanzania, mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na asizidi miaka 30.
Wakati huohuo, Umoja huo umesogeza mbele uchaguzi mkuu wa ngazi za wilaya ili kupisha sensa na Sikukuu ya Eid El Fitri. “Uchaguzi wa Mkuu wa ngazi za wilaya umesogezwa mbele ili kupisha kazi ya sensa na Sikukuu ya Eid El Fitri na sasa utafanyika kati ya Agosti 28 na Agosti 30 mwaka huu. ”alisema Shigela.