Maajabu Ya Kisiwa Cha Jibondo

JIBONDO ni kisiwa kidogo katika eneo la Kisiwa cha Mafia kilichobeba jina la wilaya ndani ya Mkoa wa Pwani. Kisiwa hicho ni moja kati ya visiwa vidogo takriban vitano ndani ya Kisiwa Kikuu cha Mafia kilichopo karibu na mlango wa Mto Rufiji kuingia Bahari ya Hindi eneo la Kusini mwa Tanzania. Mbali ya Jibondo, visiwa vingine wilayani Mafia ni Chole, Juani na Bwejuu.
Wakati Wilaya ya Mafia inatajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoachwa nyuma katika maendeleo hapa Tanzania, Kisiwa cha Jibondo ambacho pia ni kijiji kimeachwa nyuma zaidi  katika maendeleo mbali na fursa zilizopo. Kwa mujibu wa wakazi wa Jibondo maana na jina hilo ni jiwe kubwa na ndivyo kilivyo kisiwa hicho, kwani kipo juu ya mwamba.Kijiji hicho ni cha asili na kimekuwepo kwa zaidi ya karne tatu huku wenyeji wake wakiwa ni Wamatumbi na Washirazi. Hata hivyo, kwa sasa Jibondo kuna makabila mengine ikiwamo Wamakonde, Wandengereko na makabila mengine yenye asili ya Pwani.
Hali ya miundombinu kisiwani Jibondo siyo ya kuzungumzia kwa kuwa hakuna umeme zaidi ya umeme wa jua unaoonekana katika jengo la Zahanati ya Jibondo, hakuna barabara, pikipiki wala gari ingawa hali hiyo pengine inachangiwa na eneo kilipo kisiwa hicho, ukubwa wake au uhalisia.
 “Jibondo ni kijiji cha asili kipo kwa zaidi ya miaka 300 na wakazi wake hata wahamiaji ni wavuvi,” anaeleza Hassan.Ardhi ya kisiwa hiki imefunikwa kwa jiwe zaidi ya asilimia 98 huku minazi ikizunguka maeneo ya ufukweni tu pamoja na nyasi fupi kwa uchache kwenye maeneo machache, ambazo hutumika kulisha ng’ombe na mbuzi wachache waliopo Jibondo.
Ni nadra kukuta mti wa matunda au chakula kama vile mpapai au mihogo katika Kisiwa cha Jibondo hivyo kukifanya kijiji hicho kutegemea kupata chakula chake nje ya kijiji hicho, iwe Kilindoni au kutoka jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, umaarufu wa Jibondo unatajwa na walio wengi wilayani Mafia kuwa ni kutokana na watu wake kwa kiasi kikubwa kuwa wavuvi huku wakiwa na vuguvugu la kisiasa lililo na sura mbili. Kisiwa cha Jibondo kina shule moja ya msingi iliyo na wastani wa wanafunzi 325 na walimu watatu ambapo hata hivyo Mwalimu Mkuu, Mrisho Mkungu, amepewa kazi ya uofisa mtendaji wa kijiji hivyo, kutokuwepo shuleni muda mwingi na shule hiyo kubaki na walimu wawili.