SERIKALI imewavua hadhi ya ukimbizi wakimbizi 38,050 kutoka Burundi waliohifadhiwa katika Kambi ya Mtabila iliyoko Kasulu mkoani Kigoma. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya ndani, Isaac Nantanga jana, ilisema uamuzi huo umefikiwa na Waziri mwenye dhamana Dk Emmanuel Nchimbi kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 4 cha sheria ya ukimbizi.
Kufuatana na sheria hiyo mkimbizi anapoteza hadhi ya ukimbizi endapo mazingira yaliyompelekea katika hali hiyo yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Taarifa hiyo ilisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali za Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kujiridhisha kuwa hapakuwa na sababu ya kuendelea kuwahifadhi wakimbizi hao baada hali ya amani kurejea nchini kwao.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa baada ya kuwavua hadhi ya ukimbizi, raia hao wa Burundi watasaidiwa kurejea kwao kwa hiari hadi Desemba 31 mwaka huu na kusisitiza kuwa watakaokaidi agizo hilo watachukuliwa hatua kama wahamiaji haramu.
Mapema Julai, mwaka huu wakati Waziri Nchimbi akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake kwa mwaka mpya wa fedha 2012/13, alisema Serikali inakamilisha taratibu za kuwarejesha makwao wakimbizi wapatao 40,000, wengi wao kutoka Burundi, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, Tanzania ilikuwa na wakimbizi 112,645 wakiwamo Warundi 48,195, Wakongo 62,632, Wasomali 1,548 na wakimbizi wa mataifa mengine 270.
Alisema hatua ya kuwarejesha makwao wakimbizi itawezesha kufungwa kwa Kambi ya Mtabila, Kigoma yenye wakimbizi 38,800, ambayo inapaswa kuwa imefungwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
“Katika mwaka 2011/12, idadi ya wakimbizi wa Burundi kutoka kambi hiyo waliorejea kwao ni 155 tu, hali iliyosababisha kambi hiyo kutofungwa,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Mkakati mpya wa kufunga kambi hiyo ni kwamba limefanyika zoezi la mahojiano ya kina na wakimbizi hao kwa lengo la kubaini kama wapo wakimbizi wenye sababu za msingi za kuendelea kuwapo nchini.”
Alisema mahojiano hayo yalifanyika kati ya Septemba na Desemba mwaka jana na kwamba matokeo yanaonyesha kwamba 33,705 hawana sababu za msingi za kuendelea kuwa wakimbizi na wengine 2,045 walionekana kuwa na sababu za msingi.
Zoezi la kuwarudisha kwao wakimbizi lilianza mwaka 2002 ambapo kambi za Karago, Mtendei, Kanembwa, Ndutu, Muyovosi, Biharamulo, Lukole A na B zilifungwa rasmi baada ya kuthibitika kuwa amani imerejea nchini Burundi.