BABA LEVO AJA NA NGOMA YA KUACHANA POLISI KWA UKATILI WAO

Msanii wa Kigoma All Stars ameachia ngoma iitwayo ‘Breaking News’ aliyoitunga kwaajili ya kuwachana polisi waonevu na wala rushwa.
Miongoni mwa mashairi yaliyopo kwenye wimbo huo ni pamoja na,
”tumechoshwa na polisi, hii ni vita na polisi
Kuvaa gwanda kusiwafanye msiwe binadamu
Usifanye watu wakose tabasamu
Kataa rushwa, usile rushwa rushwa ni haramu
Askari bora ni mwenye busara na nidhamu.”

Akiongea na 255 ya Clouds FM jana, Baba Levo alisema, “kuna askari wachache ambao wanachafua jeshi la polisi, yaani wanafanya vitu ambavyo viko tofauti, wanawasingizia watu kesi, wanachukua rushwa, wanawaachia watu, watu wanatoka ambao wana makosa ya kweli, sasa wamejikuta wametengeza chuki na raia, yaani raia hawawapendi askari tena, kitu ambacho ni kibaya sana. 


Askari anatakiwa ashirikiane na raia ili aweze kupata data za mtaani, kwasababu sisi raia tuko mtaani ndio tunajua nani mwizi, nani sio mwizi, nani anaingia saa ngapi, sisi ndo tunaweza kumpa data askari, ndio kitu kikaitwa polisi jamii au ulinzi shirikishi.

 Lakini ulinzi shirikishi haufanikiwi sababu askari wanatupiga. Wewe umenipiga jana halafu leo hii unataka nikupe data, ntakupaje? Haiwezakani.” 


“Nimeandika ngoma hii kwa uchungu kwasababu mimi baba yangu alikuwa ni askari pia na baba yangu mimi aliuawa na raia.

 Kwahiyo unakuta makosa ya askari wengine yanaweza kuwaponza askari wengine sababu raia wanachukulia ni wale wale. Siwezi kujua baba yangu alikuwa mwema kiasi gani au alikuwa mbaya kiasi gani sababu ni vitu ambavyo vilikuwa moyoni mwake, lakini kwa mimi navyomjua baba yangu alikuwa ni mtu safi, lakini aliuawa.”

Akisimulia jinsi baba yake alivyouawa Baba Levo alisema, 


“story huwa sipendi kuifuatilia sana kwasababu naonaga inaniumiza lakini baba yangu alikuwa ni mkuu wa kituo, alikuwa ni copro. Siku moja ilikuwa ni Jumapili mimi niko zangu nacheza cheza mchangani, siku hiyo mapema mapema akawa anatoka anaenda kanisani, wala siku hiyo nadhani hakuwa na mpango wa kwenda kazini. Akanipita.


Usiku sasa mimi nimelala, Jumapili hiyo usiku nikasikia watu wanalia. Nikajiuliza kwanini watu wanalia, nikatoka, nilivyotoka nikamuuliza bibi kuna nini? Akaniambia baba yako amefariki. Nilikuwa bado mdogo mdogo ndio nimemaliza la saba.


Nikawa najiuliza baba amefariki vipi wakati amenipita asubuhi hapa alikuwa haumwi hana tatizo lolote. Baadaye ndio nilipata taarifa kwamba alipotoka kanisani alipitia kituo cha mjini pale Kigoma mjini kama sijui kuongea na rafiki zake sijui kwenda kufanya nini. 


Akajikuta kuna mtu alitakiwa apewe kazi ya kufuatilia sijui kesi gani kuna sehemu moja panaitwa Mkongolo, jamaa alikuwa hajafika kwahiyo akajikuta yeye ndio anapewa hiyo kazi aende kule, alikuwa yeye na rafiki yake. 


Wakapewa silaha wakawa wameenda huko, walipofika sijui walishindwa kuelewana nini na wanakijiji, basi wanakijiji wakawa wamewazuia, wakawa wamewaua. Mpaka leo ina miaka kama 13 lakini sitakagi kuifuatilia kiundani najua inaweza ikaniumiza sana moyo wangu.”