Na: Mwandishi
wa Thehabari.com
SEKRETARIETI
mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya
uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa
kwenye chaguzi za chama hicho vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa
imezoeleka.
Kauli hiyo
ya viongozi wa juu wa CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti
Tanzania Bara (Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa
jana na viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam
katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi hiyo
tena.
Akizungumza
na umati wa wanachama hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya
ziada ya kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo haiko kama
ilivyokuwa zamani.
“Lazima
kujiuliza nini kimekifanya chama hiki kufikia hapo kilipo na kuangalia nini cha
kufanya ili kuondokana na hali hiyo. Pale mnapohisi hali ya kuungwa mkono
inapungua lazima tujiulize, kulikoni..! Nini cha kufanya ili kuimarisha chama,”
alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha wanakijenga chama na
kuimarisha zaidi ili kiendelee kuwaongoza Watanzania.
“Chama chetu
hakifanyi mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa tutatengeneza
utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao wanafanya kazi
yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ipo
haja ya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na propaganda hasi za baadhi
ya vyombo vya habari na wapinzani ili kukabiliana na hali hiyo. Aliwataka
wanaCCM kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa yakikigawa chama hicho.
Awali
akizungumza Kinana alisema vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha
vinakoma mara moja ili kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na
tuhuma za wachache dhidi ya vitendo viovu.
Alisema
chini ya uongozi wake atahakikisha mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM
yanaondoka kwa kuwaengua wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na
vitendo vinavyo leta sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi
kuiongoza nchi yetu wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka
akisimama mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM
kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa?
Aliwataka
wana-CCM kushirikiana katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi jukumu
hilo, ambalo wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano hayo.
Alisema CCM
ina wanachama milioni 5 ambao asilimia 99.9 wengi wakiwa ni masikini na
waadilifu huku asilimia 0.1 wakiwa ni wala rushwa wakubwa, wapenda mizengwe,
wapendeleaji hivyo kujikuta idadi hiyo ikikichafua chama chote jambo ambalo
alisema chini ya uongozi wao hawawezi kuacha hali hiyo iendelee.
Alisema
atahakikisha anasimamia ilani ya chama vizuri huku kanuni mbalimbali zikifuatwa
ili kuleta haki ndani ya chama hicho, alisema kuna kazi kubwa ya kukijenga chama
hicho,
Alisema
pamoja na viongozi wenzake watahakikisha baadhi ya wana-CCM waliokuwa na tabia
za mizengwe pamoja na kupanga safu za viongoli ili kubebana kimaslahi inatoweka,
hivyo kumtaka kila mwanachama afanye kazi ya kumuingizia kipato na si kutegemea
kunufaika na nafasi ya uongozi.
Naye Makamu
Mwenyekiti Bara, Mangula alisema wapo baadhi ya viongozi wameingia ndani ya
chama kwa rushwa na tayari malalamiko juu ya mizengwe ya uchaguzi wa chama hicho
uliofanyika yamewafikia, hivyo kwa sasa wataanza kupitia kwa kina kila
malalamiko na atayebainika kuingia kwa rushwa ataenguliwa bila kumuogopa.
“Tunajipa
miezi sita ndani ya miezi sita walioingia kihalali wataendelea lakini walioingia
hovyo hovyo ‘out’…walioingia kwa pesa nje, hata wale waliokuwa wanatumwa
vibahasha nao tukiwajua wale nje, hatukubali chama chetu kituhumiwe kwa rushwa,
wala hatuta ngoja ushahidi sijui wa TAKUKURU, Polisi hakuna tutakisafisha Chama
Cha Mapinduzi,” alisema.
“…Lakini na
nyingi mliokubali kununuliwa kama sambusa mlifanya makosa, tusikubali
tena…kwanini mtu ukubali kuthaminishwa kama sambusa?,”