Majambazi Waliojeruhi Mapadri Watiwa Mbaroni


Na:  Geofrey Nyang’oro


WATU wanne akiwamo mwanamke mmoja wanaodaiwa kuwavamia na kuwajeruhi mapadri wawili kwa risasi na nondo mkoani Iringa, wamekamatwa.

Watuhumiwa hao ambao ni wakazi wa Ismani wanahusishwa na matukio mawili ya ujambazi uliofanyika katika Parokia za Kanisa Katoliki lililopo eneo la Kihesa Iringa Mjini na Parokia ya Isimani iliyoko Iringa Vijijini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda aliwaambia waandishi wa habari ofisni kwake jana kuwa watuhumiwa wote wamekamatwa kufuatia msako makli uliofanywa na polisi baada ya tukio hilo lililsababisha watu watatu kujeruhiwa.

Alisema nyumbani kwa mwanamke ndiko walikuta bunduki iliyotengenezwa kienyeji inayodaiwa ilitumika katika ujambazi huo.

“Upekuzi uliofanyika nyumba kwa nyumba katika nyumba ya mwanamke ikipatikana gobore iliyotumika kutekeleza uhalifu huo. Nyumba ya mtuhumiwa mwingine motto wa mwanamke huyo zilipatikana gorori 37 na gramu 100 za baruti,” alisema.
Katika matukio hayo watuhumiwa wanadiwa kupora Sh4 milioni na Euro 100, huku wakiwashambulia kwa mapanga na risasi mapadri wawili, Padri Anjelo Burgio (66) wa Paroko wa Parukia ya Isamani na Msaidizi wake, Padri Herman Myala (36).
Mwingine aliyejeruhiwa kwenye matukio hayo ni Mlinzi wa Kanisa la Kiaskofu la Kihesa, Batholomeo Nzigiliwa.

Hali za majeruhi
Kamanda Kamuhanda alisema majeruhi wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa  ya Mkoa wa Iringa na kwamba mlinzi wa Kanisa la Kihesa Nzigilwa hali yake ikielezewa kuwa ni mbaya.

Alisema mapadri  Burgio na Myala, wote wanaendelea vizuri.
Kamanda huyo alisema kuwa wanaendelea kuwasaka watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo.