KWELI kufa kufaana, baadhi ya wapigapicha wa kujitegemea
jijini Dar wamehamia katika kaburi alilozikwa staa wa filamu za Kibongo,
marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’ lililopo kwenye makaburi ya
Kinondoni kwa lengo la kuwapiga picha watu wanaolizuru kisha kuwatoza fedha.
Tukio hilo lilishuhudiwa na mpekuzi wetu Aprili 13, mwaka
huu baada ya kuwakuta wapigapicha hao wakiwapanga foleni waombolezaji na
kuwaambia watapigwa picha na wao watatakiwa kulipa fedha ili kuzikomboa.
Mpekuzi wetu alimuuliza mmoja wa wapiga picha hao kiasi
wanachotoza kwa kila picha moja ambapo alijibu ni Sh. elfu mbili (2,000).
“Ndiyo utaratibu wetu, mtu yeyote anayetaka kupiga picha
kwenye kaburi la Kanumba hata kama atakuja na kamera yake, lazima atulipe elfu
mbili,” alisema mpigapicha huyo.
Akaendelea: “Unajua kila mtu ana staili yake ya kumuenzi
kipenzi chake pindi anapofariki dunia, sasa kwa sisi tumeona hii ndiyo staili
yetu, kwanza tunalilinda kaburi maana kila tunapokuja asubuhi cha kwanza
tunafanya usafi ndipo tunaanza kutoa huduma ya kupiga picha kwa dau hilo.”
Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 7, mwaka huu
nyumbani kwake maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza jiji Dar.