BADO sakata la kifo cha Steven Charles Kanumba ‘The Great’
ni bichi na kwa mambo yalivyo, kuna uwezekano watu wengi zaidi wakaingia
matatani kwa namna moja au nyingine.
Habari zinadai kuwa wakati upelelezi ukiendelea, kuna ambao
tayari wamehojiwa na inawezekana wengi watahojiwa kwa kadiri ishu hiyo
inavyozidi kuchukua sura mpya.
WALIOHOJIWA
LULU
Ukimwondoa mtuhumiwa namba moja wa kifo hicho, Elizabeth
Michael ‘Lulu’, ambaye alishahojiwa na kupandishwa kizimbani kisha kuwekwa
nyuma ya nondo za mahabusu ya Segerea, Dar, kuna wengine walio roho juu.
SETH BOSCO
Katika tukio hilo, pia tayari ndugu ambaye ni mdogo wa
marehemu Kanumba, Seth Bosco naye alishafikishwa kwenye kituo cha polisi cha
Oysterbay Kinondoni na kuhojiwa kuhusu anachokijua juu ya kifo hicho kwa kuwa
ndiye mtu wa kwanza kuingia chumbani baada ya staa huyo kudondoka.
DAKTARI
Naye aliyekuwa daktari wa marehemu Kanumba aliyetajwa kwa
jina moja ka Kabugi maarufu kama Kidume, alikuwa mmoja wa watu waliofika kituo
cha polisi Oysterbay kutoa maelezo akiwemo mwigizaji swahiba wa marehemu
Kanumba, Vincent Kigosi ‘Ray’.
RAY
Pamoja na kuwa mmoja wa watu waliokwenda kutoa maelezo
polisi siku ya tukio la kifo cha Kanumba Aprili, 7, mwaka huu, mwishoni mwa
wiki iliyopita Ray alizua gumzo baada ya kupamba ukurasa wa mbele wa gazeti
moja litokalo kila siku akikanusha kuhusika na kifo hicho.
Swali kwa Ray lilikuwa ni nani aliyemwambia kuwa kahusika
hadi akanushe hivyo kumjengea picha ya tofauti kwenye jamii.
ALI KIBA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, staa wa Bongo Fleva, Ali Saleh
Kiba, naye alisikika akikanusha kuwa si kweli kwamba alihojiwa juu ya sakata
hilo kufuatia madai kuwa ndiye aliyempa lifti Lulu wakati anaondoka kwa Kanumba
baada ya tukio hilo.
WENGI ZAIDI KUINGIA MATATANI
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kindoni, Charles
Kenyela alipokuwa akifunga mjadala huo na kuachia Kitengo cha Upelelezi wa
Makosa ya Jinai kifanye kazi yake, katika sakata hilo watu wengi watahojiwa
kwani watafuatilia vyanzo mbalimbali ikiwemo simu za Kanumba na Lulu kujua watu
waliowasiliana nao wahojiwe wanahusikaje na tukio hilo.
‘KUFA KUFAANA’ NAO MATATANI
Mbali na kesi ya mauaji ya Kanumba, pia waliotumia kifo cha
Kanumba kujitajirisha (kufa kufaana) kwa kuchuuza bidhaa mbalimbali za msanii
huyo mkubwa ndani na nje ya nchi, nao wameingia matatani kwa kukamatwa na
kutiwa mbaroni.
Bidhaa ambazo zilipigwa marufuku kuuzwa na shirikisho la
filamu nchini (TAFF) ni pamoja na nguo, vitabu na mikanda ya mazishi ya Kanumba
hivyo kila aliyekamatwa na ‘prodakti’ hizo aliingia matatani.