KAMATI YA MAZISHI YA MSANII STEVEN CHARLES KANUMBA
Taarifa kwa vyombo vya habari
APRILI 9, 2012
Msanii
wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia
kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7,
2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es
Salaam.
Mazishi
ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu,
mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa
fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia
ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.
Mpangilio
wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki
mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la
kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito
unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.
RATIBA
Mwili
wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali
ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa
Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni
ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya
watu wote kumuaga.
Wito
unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi,
wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi
ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda
Leaders Club.
Saa
3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders,
ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali
ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Saa
4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa
5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.
Saa
6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri
na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara
kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita
Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea
makaburini.
Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.
Kamati
ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika
ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani
aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake
ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.
K.N.Y GABRIEL MTITU
MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI