UCHAMBUZI: HAYA NDO MAMBO MANNE AMBAYO "WAPENZI" WANATAKIWA KUJIFUNZA KUTOKANA NA KIFO CHA STEVEN KANUMBA


KWANZA namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia siha njema na pia kunipa mwangaza wa kuandika hiki ninachokusudia. Nawakaribisha sana!

Labda kwa wale wasiofahamu niwaambie tu kwamba dhana ya mapenzi ni dhana yenye wigo mpana sana na ndiyo maana hutasikia hata siku moja tumepumzika kuizungumzia. Hata hivyo, tunachofanya siku zote ni kukumbushana kwa yale tunayoyafahamu na kushauriana pale tunapohisi wengi hufanya makosa.

Mpenzi msomaji wangu, bado tuko kwenye majonzi kufuatia kifo cha msanii ambaye alikuwa kipenzi cha wengi, Steven Kanumba. Ni kifo kilichowashitua wengi lakini pia kinaweza kikawa kimewagusa wengi walio katika uhusiano wa kimapenzi.

Katika maelezo ya awali inaonekana kuwa Marehemu na Lulu walikuwa wapenzi kwa siri sana.
Siwezi kuhoji ni kwa nini ilikuwa hivyo kwa kuwa kila mmoja ana maamuzi yake ila nimeshawahi kuzungumzia madhara ya kuwa katika uhusiano wa kimapenzi wa siri.

Sasa hivi ni kitu cha kawaida kwa mwanaume kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na msichana kisha akamuambia hataki uhusiano wao ufahamike kwa watu huku akitoa sababu anazozijua mwenyewe. Mimi sipingi hilo kwa sababu hata walio kwenye ndoa walianza kwa siri na mwishowe uhusiano ukawa wazi na kuoana.

Ninachotaka kizungumzia hapa si uhusiano wa siri uliokuwepo kati ya Lulu na Kanumba bali nataka kuelezea mambo manne ambayo tunaweza tukajifunza kwenye tukio hili hasa kwa wale walio katika ndoa na uhusiano wa kawaida.

Usaliti
Hakuna kitu kinachouma katika maisha ya kimapenzi kama kusalitiwa. Wapo waliofikia hatua ya kujiua ama kuua baada ya kusalitiwa na wapenzi wao waliotokea kuwapenda. Wapo pia waliochanganyikiwa na kushindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku kama inavyotakiwa kwa sababu ya kutendwa.

Ukisikiliza maelezo yaliyosababisha ugomvi kati ya Lulu na Kanumba, tunaambiwa Lulu alikuwa akizungumza na mtu aliyesadikiwa kuwa ni mwanaume kwenye simu. Kwa nini Kanumba alimvaa Lulu? Ni kwa sababu alisikia uchungu kuhisi anaibiwa mali zake na ndiyo maana yakatokea ya kutokea.

Kwa maana hiyo sisi tulio katika ndoa au kwenye uhusiano wa kawaida tuwe makini katika maisha yetu ya kila siku. Tufahamu kuwa usaliti unaweza kusababisha kifo kati ya wawili waliotokea kupendana.

Subira
Siku zote hasira ni hasara na subira yavuta heri. Mpenzi wako anapokutendea jambo baya usikimbilie kufanya maamuzi mabaya. Unatakiwa kuwa na moyo wa subira na kulikabili suala hilo kwa utulivu bila jazba.

Kama umekuta sms isiyoeleweka kwenye simu ya mpenzi wako au umekuta mke wako anaongea kwenye simu na mwanaume, usikimbilie kufoka au kumpiga. Kumbuka kukosa uvumilivu katika mazingira hayo unaweza kujikuta unarusha kofi na hilo tu likatosha kumtoa uhai mpenzi wako kisha ukaanza kujuta.

Ugomvi
Katika saikolojia ya mapenzi, kupigana kwa wawili waliotokea kupendana si kitu kizuri. Kama utamwambia mpenzi wako kuwa unampenda kisha kesho yake ukamzaba vibao kwa kosa dogo, hiyo itadhihirisha unafiki ulionao. Ni kweli kuna suala la wivu na hasira lakini tunachotakiwa kufanya ni ‘kujikontroo’.

Kupigana kunapunguza mapenzi, kupigana kunaweza kusababisha kifo, sasa kama kweli unampenda kwa nini umpige? Hata kama amekukosea hutakiwi kufanya hivyo.

Ndiyo maana unaweza kuona ni kwa jinsi gani Lulu amemkosa Kanumba ambaye huenda walipanga kuoana kwa ugomvi ambao kila mmoja angekuwa makini yasingetokea yaliyotokea.

Hili liende moja kwa moja kwa wanaume wanaojifanya wababe kwa wapenzi wao. Wapo wanandoa ambao haipiti siku bila kupigana, hii siyo sawa na wanaofanya hivyo wajue mbali na kujishushia heshima mbele ya jamii lakini pia wanaweza kufupishiana maisha.

Utii kwa mpenzi wako
Ukifuatilia sana utabaini Kanumba alimkalisha Lulu chini na kumweleza kuwa wawe wapenzi lakini iwe siri hadi pale atakapoona ni muda sahihi wa penzi lao kuwa wazi.

Kuonesha kuwa Lulu alimpenda sana Kanumba na hakuwa tayari kumkosa katika maisha yake, alitii hilo na hata siku za hivi karibuni alipokuwa akihojiwa na Salama Jabir katika Kipindi cha Mikasi kinachorushwa kwenye Runinga ya EATV, alisema hana mpenzi.

Alisema hivyo akijua kabisa anadanganya lakini alikuwa hana jinsi kwani alikuwa akitii kile alichoambiwa na mpenzi wake.

 Wewe pia uliye katika uhusiano unatakiwa kumtii mpenzi wako, anachokuambia kama hakina madhara ni vyema ukakitii kwani ni ishara kwamba unamheshimu na kumpenda.

Kwa leo ni hayo tu niliyotaka kuzungumza, niseme tu kwamba tuwe watu wa kujifunza kutokana na matukio na tuwe tayari kubadilika ili tuweze kuishi kwa amani na furaha.