HIZI NDO KAULI ZA VICENT NYERERE ZILIZOIUMBUA TBS BUNGENI

Picture

Vincent Nyerere (Mbunge)

Katika Mkutano wa Bunge uliomalizika, Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema), alilipua mbinu zilizofanywa na ‘wakubwa’ wa TBS kwa kujiundia kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi na kuliibia taifa mabilioni ya shilingi. Yafuatayo ni maneno aliyoyazungumza bungeni.

Nashukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika. Kwanza nipende kumshukuru Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Naibu wake, Mheshimiwa Kabwe Zitto, kwa kunipa ujasiri wa kufuatilia yale ambayo wenzetu kwenye Kamati walikuwa wakifuatilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nichangie sehemu nyingine, lakini nimeona nijikite kwenye TBS. Nimeshangaa sana majibu niliyoyapata jana kwenye swali nililouliza namba 62, Wizara ikanipa majibu ya uongo na niliyakataa hapa na nikamwuliza Naibu Waziri kama tutaleta ushahidi, kwamba baadhi ya watumishi wa Wizara yako wanahusika na hizi kampuni hewa uko tayari kujiuzulu? Hakunijibu. 

Na nilikuwa naomba niweke wazi, tarehe 25 mwezi wa tisa mwaka 2007 Movenpick (Dar es Salaam) walikaa kikundi cha watoto wa mjini wakatengeneza kampuni hiyo wakagawana dili. Wakatengeneza makampuni ya ukaguzi wa magari wakisema kwamba ni makampuni ya nje siyo ya nje.

Kampuni ya WTN ya UK, ya mtani mmoja anaitwa Wilson Mtabagi. Kuna kampuni Dubai inaitwa JK (Jabali Kilimanjaro), mwenyewe ni Rashidi Kimwanga.

Barrick Garage ya Hong Kong, mwenyewe ni Abdul Lutashi. Na Mbunge wake yuko hapa wa Mafia. EAA ya Japan, Prosper Nguku, Mbunge wake yule pale. Zakur Mohamed Al-Garage, Said Aboud, Zanzibar. Tariff Automotive Shamir Kuwey wa Zanzibar. Kwa hiyo nilikuwa nasema - namaanisha ni uongo.

Kwanza hakuna magari yanayokaguliwa na watu hawa. Kwenye jibu la Waziri, sehemu ya jibu anasema magari mengine yanaweza kuwa na mionzi yenye athari kwa binadamu. Hakuna hata mtu mmoja anakagua mionzi kwenye gereji. Zote hizi zimeshafika zingine hazipo. Mwaka 2002 wakati wanaanza kukagua, mwaka 2003 Total Automotive ya Dubai ambayo inafanya kazi ya local kukagua magari, ilikuwa inafanya kazi vizuri sana. Waliwanyima kazi hiyo kwa sababu hawakuwa tayari kutoa kitu kidogo.

Ndiyo kampuni zingine hizi zikatengenezwa. Kulikuwa kuna kampuni Hong Kong inaitwa Fin Dabi, ilikuwa inafanya kazi vizuri ya kiserikali. Kwa sababu ilikuwa inafanya kazi vizuri ya kiserikali, kwa sababu ilikuwa hawawezi kutoa kitu kidogo (rushwa) wakaiacha. Akapewa bwana mmoja Kigamboni anaitwa Cassian Mbagate afanye kazi hiyo. Hakuleta fedha, akanyimwa kazi hiyo wakampa huyu kijana wa Quality Garage. Hana gereji hana chochote.

Na nashangaa tarehe 10 mwezi wa pili wakati Tea Gate wanaleta ripoti hapa, wakaleta picha za uongo ambazo wanatuonyesha kwamba kuna gereji pale na kuna wakaguzi. Bahati mbaya mimi ni mwenyeji sana hapa duniani japokuwa sikuzaliwa zamani, nikawaambia watu hawa hii ni gereji ya MM Auto Part. Mkiendelea kudanganya hivi tutawaumbua na CAG tarehe 15 mwezi wa pili wakapeleka ripoti nyingine. Bahati ile ripoti ya zamani ninayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja ilikuwa ni kwamba haya magari hayakaguliwi. Nina ushahidi kwa chassis number, yapo magari ambayo tumeyaingiza hayakukaguliwa kwa sababu kampuni hazipo. Lakini yalitumiwa certificate.

Bahati nzuri wakati Mheshimiwa Zitto Kabwe anawatuma wabunge waende wakakague kama kampuni ipo, waliuziwa certificate hata gari hawana. Hii habari ya kusema kwamba ukaguzi wa magari unazuia fedha zisiende nje ni uongo. Fedha zinaenda nje zinarudi hapa hapa watu wanagawana.

Kwa hiyo nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri, inawezekana hujui. Mimi nilikuwa nadhani ungetuita wakati jana naongea na Chief Whip ukaniuliza nikusaidie nini cha kufanya na the way forward. Wewe ukang’ang’ana kubisha. Aibu. Mheshimiwa, kampuni nyingine ambayo haifanyi ukaguzi ni hii ya GAAN.

Niliwahi kununua gari ambayo ilipata usajili wa namba T 410 ADA.

Ikapewa certificate ya kukaguliwa na nilinunua online. Ikaja hapa ina matairi ya slow, nikabadilisha. Tanzania hakuna slow kama walikagua gari ile isingeingia hapa. Kwa hiyo tunavyosema magari hayakaguliwi tunamaanisha hayakaguliwi na kampuni hizi siyo za nje ni za watu wa hapa hapa, tunawajua mpaka wanapoishi.

Kwa hiyo nilikuwa napenda… ni vizuri watu hawa tungewashauri wayafungue makampuni hayo hapa, wakagulie hapa ili watu wetu wapate ajira kuliko kudanganya na kupoteza fedha nyingi sana za kigeni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia fedha ambazo makampuni haya yamekusanya tangu wameanza kukagua magari ni dola milioni 18. Lakini sisi tumepata dola milioni 2.2 peke yake, nyingine zote wamegawana watu wengine.

Halafu tumekaa tuna matatizo, shule hazina madawati. Watu wanakula hela, halafu watu wako hapa wanacheza sarakasi na taulo - watabaki uchi!

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninakushukuru. Naomba muda wangu nimwachie Mheshimiwa Deo Filikunjombe kwa sababu yeye alikwenda kule na Kamati. Mimi nimekuwapo kule tangu miaka ya 1990, najua kila kitu, namjua kila mtu. Waziri akitaka the way forward niko tayari kumsaidia kwa sababu niliapa kusaidia Taifa hili. Nashukuru sana. Naunga mkono hoja za Kamati.